Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora kabisa.
Ni kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UJASIRI NA UTHUBUTU…
Hivi ni vitu viwili ambavyo unahitaji kuwa navyo ili kuweza kufanikiwa.
Unahitaji kuwa jasiri ili uweze kuishinda hofu.
Unahitaji kuwa na uthubutu ili uweze kujaribu mambo mapya, uweze kuhoji na hata kuuliza maswali.
Dunia haipendi vitu vinyonge, ndiyo maana ujasiri ni muhimu sana.
Bila ujasiri hofu itakuzuia kupiga hatua yoyote.
Wale unaowaona wakipiga hatua siyo kwamba hawana hofu, wanazo, ila ujasiri wao unazizidi hofu.
Na kama unavyojua, lolote lenye manufaa, pia lina hatari. Kutaka kuepuka hatari maana yake usifanye lolote kubwa na lenye manufaa.
Ujasiri unatengenezwa, kwa kuwa na sababu kubwa zaidi za kufanya kitu kuliko hofu zinazokuzuia kufanya.
Uthubutu unatengenezwa kwa kujiwekea utaratibu wa kujaribu mambo mapya, kuongea na watu wapya, kuuliza maswali mazuri.
Usiseme ulizaliwa bila ujasiri au uthubutu,
Kiri umefundishwa kutokuwa jasiri, na anza kufanyia kazi ujasiri wako.
Kwa sababu bila ujasiri na uthubutu, hakuna kikubwa unaweza kufanya.
Maana dunia yenyewe haitakuachia upige hayua hata ndogo.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.