Rafiki,

Nina imani upo vizuri kabisa, ukiendelea kuweka juhudi kubwa ili kuweza kutengeneza matokeo makubwa kwenye maisha yako. Hilo ndilo jambo la msingi kufanya, na mimi rafiki yako nahakikisha wakati wote nakupa mbinu bora za wewe kuweza kufanikisha hilo.



Leo nimekuja kukukumbusha jambo moja ambalo huenda hujawahi kuliangalia vizuri. 

Jambo hili linahusu matatizo unayoyatengeneza kwenye maisha yako mwenyewe, kutokana na tabia yako ya kufuatilia maisha ya watu.

Kila mtu, kwa namna moja au nyingine, huwa kuna wakati anafuatilia maisha ya wengine. 

Iwe ni kwa uzuri kutaka kujua mambo yanaendaje na mara nyingi zaidi ni kwa ubaya kutaka kujua mtu anakosea wapi, au kutaka kuona mtu anaishia wapi, hasa pale anapofanya jambo ambalo hatujazoea kuona likifanywa.

Watu wamekuwa wakitumia sehemu kubwa ya maisha yao kwenye hilo la kufuatilia maisha ya wengine, na imekuwa inawagharimu kwa kiasi kikubwa. Huwa hawaoni hilo haraka kwa sababu hawajawahi kukaa chini na kutafakari wanachopoteza kwa kuweka juhudi kubwa kufuatilia wengine.

Leo nimekuandalia mambo manne mabaya unayoyatengeneza kwenye maisha yako, kutokana na tabia ya kufuatilia maisha ya wengine. Nakushirikisha siyo kukutisha, bali kukuwezesha kufanya maamuzi sahihi yenye manufaa kwenye maisha yako. Karibu sana tujifunze na kuweza kuchukua hatua.

1. Kuingia kwenye maisha ya maigizo ambayo wengine wanaishi.

Unajua kwa nini watu wanapenda kuangalia maigizo na tamthilia, kuzifuatilia kwa karibu japokuwa wanajua siyo ukweli? Kwa sababu watu wanapenda maigizo, watu wanapenda hali ya kuigiza kwenye maisha yao pia.

Mambo mengi ambayo watu wanafanya kwenye maisha yao, ni maigizo. Matatizo mengi ambayo watu wanayo kwenye maisha yao, wameyatengeneza wao wenyewe. Sasa wewe unapochukua muda wako na kuanza kufuatilia mambo ya wengine, unakuwa umejiingiza kwenye maigizo haya.

Sasa habari mbaya kwako siyo kuingia tu kwenye hayo maigizo, bali ni hayo maigizo huwa hawaishi. Kila wakati kuna jambo jipya, kila siku kuna kitu kipya cha kufuatilia. 

Kama wale wanaofuatilia maisha ya wasanii, kila siku huwa hawakosi kufanya jambo jipya na la ajabu la kuwafanya watu wawazungumzie. Hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wengine pia, wanapenda kutengeneza maigizo ambayo yatawafanya wengine wawaangalie.

Kwa mfano kuna watu unaweza kuona kila wakati wana matatizo, likiisha moja, linakuja lingine, na yote utaona unahusika moja kwa moja. Hayo ndiyo maisha ya maigizo ambayo ninayazungumzia. Usiposhtuka haraka na kuondoka, kila wakati utajikuta kuna jambo la kufuatilia au kusaidia kwenye maisha ya wengine, huku ukikosa muda wa kufanya mambo yako kwa umakini.

2. Kutoa ushauri mbaya.

Kwanza kabisa nikuambie jambo moja, hakuna mtu anataka ushauri wako kama unavyofikiria. Kwa kifupi watu hawajali sana kuhusu maoni yako, wapo bize na maigizo ya maisha yao. Hivyo unapojihusisha na maigizo hayo, huwa unajikuta ukitoa ushauri ambao siyo mzuri na pia hauhitajiki.

Kama nilivyokuambia, kuna watu unawaona kila wakati wana matatizo au changamoto, ukafikiri wanakazana kweli kuwa na maisha bora, kumbe wenzako hicho ndiyo kitu wanachofurahia kwenye maisha yako. Hivyo ushauri wako huwa hauhitajiki na wakati mwingine kuonekana hauna maana.

Usikimbilie kutoa ushauri au maoni yako juu ya maisha ya wengine, kama wao wenyewe hawajataka wewe ufanye hivyo. Na ukishaacha kufuatilia maisha yako, hutapata hata huo muda wa kuanza kutoa ushauri ambao hauhitajiki.

3. Kupoteza muda ambao ungeutumia vizuri kwa mafanikio.

Muda unaotumia kufuatilia maisha ya wengine, ungeuelekeza kwenye shughuli zako, ungeweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Muda ambao unatumia kuangalia wengine wamefanya nini, nani kasema nini, nani kakosea wapi, ungeuweka kwenye kujifunza zaidi kuhusu kazi yako, biashara yako, kutafuta wateja wapya, kufanya kazi za ziada, ungekuwa mbali sana.

Kwa kujitolea kufuatilia maisha ya wengine, umekuwa unajizuia wewe mwenyewe kufanikiwa. Na kama nilivyokuambia hapo juu, maigizo ya watu huwa hayaishi, hivyo unajikuta kila siku kipo kitu unafuatilia kuhusu wengine.

Badili muda huo na upeleke kwenye shughuli ambazo zinakuzalishia, zinakuwezesha kupiga hatua na kuwa mtu bora zaidi.

4. Kujishushia heshima yako.

Hili ndiyo baya zaidi kuliko yote. Iko hivi, unapokuwa unafuatilia maisha ya wengine, kuna wakati utajikuta unatoa maoni yako, ukiona unafanya vizuri au unashauri kitu kizuri. 

Lakini watu wakachukulia unachofanya siyo kizuri na ukaonekana wewe ni mtu mbaya.

Kwa mfano kuna mtu anakosea mambo anayofanya kwenye maisha yako, kwa kuwa unamfuatilia na kuona hayo, mnakuwa kwenye maongezi na mtu mwingine, mara mada inahamia kwa yule anayekosea, na wewe unatoa maoni yako kwamba hakupaswa kufanya jambo fulani alilofanya. Mtu yule anaweza kutoka kwako, akakutana na mtu yule na kumweleza maoni yako, na yeye kwa kuwa anapenda maigizo zaidi, anakuchanganya na wewe kwenye maigizo yake. Anaanza kuona mlikuwa mnamsema, au mnamfuatilia mambo yake na kadhalika. Hilo linaweza kupelekea yeye kukusema vibaya kwa wengine na kusababisha heshima yako kushuka.

Rafiki yangu, kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako kinapaswa kuwa wewe. Acha kabisa kuweka muda wako kufuatilia mambo ya wengine, labda kama wamekuja kwako na kukuomba uwasaidie kwenye jambo fulani. Tofauti na hapo, utakuwa salama kama utakazana na maisha yako na kuacha wengine waendelee kufanya yale wanayofanya. 

Puuza hili na utapoteza muda mwingi kufikiria unawasaidia wengine kumbe unajipotezea wewe mwenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.