Kuna kosa moja kubwa sana la muda ambalo watu wengi wanaoingia kwenye biashara huwa wanalifanya. Kosa hilo ni kujikadiria muda mdogo wa biashara kuweza kusimama yenyewe na kupata faida.

Watu wengi huingia kwenye biashara wakitegemea kuanza kutengeneza faida ndani ya muda mfupi tangu wanapingia. Lakini uhalisia umekuwa ni tofauti na matarajio. Mara nyingi, muda huwa mara mbili mpaka mara tatu ya ule ambao mtu alitegemea biashara iwe imeshasimama na kutengeneza faida.

Hivyo kama ulikuwa unafikiria biashara itakuchukua mwaka mmoja kusimama, anza kufikiria miaka miwili mpaka mitatu. Hii ni kwa sababu kuna mambo mengi ambayo huwa yanatokea wakati biashara inaanza na inaendelea, ambayo yapo kabisa nje ya uwezo wako. Pamoja na juhudi kubwa unazoweza kuweka, bado kuna mambo yanatokea ambayo huna namna inabidi tu usubiri au uende kama hali ilivyo.

Sasa hili limekuwa ni changamoto kubwa, pale mtu anapokuwa ‘amejilipua’, kama wengi wanavyosema. Yaani umeacha mambo mengine uliyokuwa unategemea na kujikita kwenye biashara. Pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea, maisha yanakuwa magumu na hilo kupelekea hata biashara kufa.

Hivyo ninachokukumbusha hapa rafiki yangu, ni unapopanga mipango yako, hasa kwenye muda, weka muda wa ziada, mambo hayataenda kama ulivyopanga mara zote.

SOMA; Kosa Moja….

Na katika hili zingatia yafuatayo;

  1. Uwe na uwezo wa kulipa gharama za biashara, kuanzia pango, kodi, mishahara na matumizi mengine madogo madogo kwa angalau miezi sita mbele. Ikiwa mwaka mmoja ni vizuri zaidi.
  2. Uwe na uwezo wa kuendesha maisha yako bila ya kutegemea biashara moja kwa moja kwa angalau miezi sita mbele. Hapo maisha yako yanaweza kwenda, yaani mahitaji yote ya maisha unaweza kuyatimiza bila ya kutegemea biashara.
  3. Uwe na uwezo wa kuiokoa biashara, pale mambo yanapokwenda vibaya. Hii ikiwa na maana kwamba kuna fedha unayo pembeni, ambayo unaweza kuiweka kwenye biashara, pale mambo yanapokwama kabisa.

Zingatia mambo hayo matatu pale unapoanza biashara, ili kukwepa kujikuta kwenye wakati mgumu mwanzoni mwa biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog