Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Ni kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kutawala kile tunachofanya.
Chochote unachofanya rafiki, kitawale, kifanye kwa kujitoa moja kwa moja na kujua kila hatua ya hicho unachofanya.
Usifanye kwa kubahatisha au kwa kujaribu,
Kwa sababu utakuwa unapoteza muda wako bure.
Amua kufanya na ufanye kweli.
Unapofanya, acha dunia ijue wewe unafanya, na unafanya vizuri sana.
Au amua kutokufanya kabisa, kama huwezi kuweka juhudi na muda unaopaswa kuwekwa.
Una uhuru mkubwa wa kuchagua kwenye maisha, hakikisha kila unachochagua, unakitendea haki. Usifanye tu kwa sababu unafanya, bali fanya kwa sababu upo tayari kutawala na uko tayari kuifahamisha dunia kwamba wewe upo na unafanya.
Kutawala unachofanya kunakuja na hatari zake pia;
💥 Utahitaji kuweka juhudi zaidi ya wengine.
💥 Utahitaji kuwa mvumilivu zaidi.
💥 Utakuwa kwenye hatari ya kupingwa na kukosolewa na wengine, kwa sababu ya hatua kubwa unazopiga.
Lakini hayo yote yasikurudishe nyuma,
Badala yake weka juhudi kubwa na Tawala, chochote chini ya hapo ni kupoteza muda.
Nakutakia siku njema ya leo rafiki, ukatawale chochote unachofanya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info