Moja ya kosa kubwa ambalo wafanyabiashara wengi huwa wanafanya, ni kutokujifunza kupitia biashara nyingine. Na hata kama wakijifunza, basi hujifunza kwenye biashara zinazofanana na zile ambazo tayari wanazifanya. Kwa njia hii huwa hawaji na kitu kipya, badala yake kuiga kile ambacho tayari wengine wanafanya.

Njia bora kabisa ya kujifunza kwenye biashara, ni kuweza kujifunza kwenye kila aina ya biashara. Ndiyo unahitaji kujifunza kutoka hata kwenye biashara ambazo haziendani na zile ambazo unafanya wewe. Hapo angalia thamani inayotolewa, jiulize kwa nini wateja wananunua pale, angalia huduma wanazopatiwa.

Unaweza kujifunza namna wateja wanahudumiwa, kujaliwa, namna wanapata thamani zaidi na hata mpangilio wa biashara ulivyo.

Kila unapoenda kwenye biashara yoyote, kupata bidhaa au huduma yoyote, usitoke pale hujajifunza chochote kuhusu biashara. Wengi hawajifunzi kwa sababu hawajui nini cha kujifunza. Hivyo wewe unachopaswa kufanya ni kujua maeneo gani ya kuangalia, maswali gani ya kujiuliza. Angalia kila kinachofanyika, kitakufundisha mengi sana.

SOMA;  Jifunze Kutokana Na Makosa Yako Na Jipange Kufanikiwa

Kwa mfano, jaribu kutembelea supermarket yoyote, zunguka kuangalia mpangilio wa bidhaa ulivyokaa. Unaweza kuona mpangilio wa bidhaa ulivyo, hazijapangwa kwa bahati mbaya, zimepangwa kwa namna ambayo mtu atashawishiwa kununua zaidi. Kwa mfano, angalia wakati unatoka kwenye supermarket, utakutana na matangazo mengi ya bidhaa zilizopunguzwa bei. Pia utaona vitu vidogo vidogo kama biskuti na vingine, vimekaa mbele yako wakati umepanga foleni katika malipo. yale yote hayafanywi kwa kubahatisha, bali lengo ni kukutamanisha wewe na kukusukuma ununue zaidi.

Yapo mambo mengi sana unayoweza kujifunza kwenye kila biashara, mazuri ya kufanya na mabaya ya kuacha. Ni wewe tu kujua unapaswa kujifunza ni i na kuhakikisha unajifunza kila unapotembelea biashara yoyote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog