Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Umeianzaje siku hii nzuri sana ya leo?
Hii ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.


Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA msingi bora na muhimu sana kwetu kwenda kupata matokeo bora kabisa.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu nafasi ya kuwa bora zaidi.
Kila tunachofanya kwenye maisha yetu, kila hatua tunayofikia, tunayo fursa kubwa ya kuwa bora zaidi. Ipo nafasi ya kuweka juhudi zaidi, ya kujifunza zaidi na ya kutoa mchango zaidi.
Hakuna mahali unaweza kufika na kusema tayari unaweza kila kitu, au unajua kila kitu. Dunia yenyewe inaenda kwa kasi kubwa, kiasi kwamba pale unapofikiri umeshafikia kilele na ukomo, ndiyo unakuwa umeanza kuporomoka.

Siku zote jipe wajibu wa kuwa bora zaidi, na kipimo kizuri kiwe jana yake, au siku iloyopita. Kuwa bora leo zaidi ya ulivyokuwa jana, wiki iliyopita, mwezi uliopita na hata mwaka uliopita.
Kazana upige hatua leo, ambayo hujawahi kupiga, ufanye kitu hujawahi kufanya na ujihisishe na watu hujawahi kuhusiana nao.

Kama kwa vyovyote vile, leo yako inafanana na jana, au wiki iliyopita, au mwezi uliopita, unafikiri upo pale pale? Labda kama unajidanganya. Lakini ukweli ni kwamba kama leo ni sawa na siku zilizopita, hujabaki pale pale, badala yake umerudi nyuma. Kwa sababu dunia inaenda mbele, hivyo kusimama kwako, kumekurudisha nyuma.

Ianze siku ya leo ukijiuliza unawezaje kuwa bora zaidi leo kuliko ulivyokuwa jana? Ukishapata jibu, fanyia kazi, chukua hayua LEO. HII.

Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info