Unapofanya biashara, hasa kwa mazingira yetu ambayo kila mtu ni mshauri wa biashara, utapata maoni mengi sana kutoka kwa kila mtu. Hata mtoto wa shule ya msingi anaweza kukushauri ni namna gani bora ya kufanya biashara yako. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanakimbilia kufanya maamuzi makubwa ya biashara zao kwa sababu ya maoni ya watu au wateja wao. Maamuzi hayo wanayofanya huwa yanakuwa siyo bora kwao wala kwa biashara zao, hivyo hupelekea biashara kuyumba.

Maoni yanaweza kuwa mazuri na ya kweli kabisa, lakini kabla hujayafanyia kazi fikiria jambo hili moja muhimu; lipi kusudi lako kubwa kwenye biashara unayofanya?

Hilo ni swali linaonekana rahisi, lakini ni zito na muhimu kulipatia jibu. Kwa sababu mara nyingi watu wa nje huwa hawajui kusudi lako la biashara, bali wao wanachoona ni njia za kupata pesa zaidi kupitia biashara yako.

Hakuna ubaya wowote kwenye kupata pesa zaidi, lakini hilo linapaswa kuendana na kusudi lako la kibiashara, ukishaanza kukimbiza pesa pekee na kusahau kusudi lako, hapo ndipo unapopotea njia, unajikuta unazo nyingi, lakini unaona bado kuna kitu hakijakaa sawa.

Hivyo angalia kama ushauri unaopewa unaendana na kusudi lako la kibiashara, kama hauendani achana nao. Watu watakushangaa unaacha hela, lakini utakuwa salama, na baadaye utapata fedha zaidi kuliko ulizoacha.

SOMA; Maamuzi Ya Mtu Mmoja….

Ukiwa na tabia ya kutanguliza kusudi la biashara mbele, hutakuja kuingia kwenye utapeli wala fedha za haraka zenye changamoto. Mara zote utafanya maamuzi sahihi kwako na kwa biashara yako. Hata pale kila mtu anakimbilia kitu na kudai ni fursa, wewe ukiona haiendani na kusudi lako la maisha, achana nalo, utakuwa salama zaidi.

Siyo kila ushauri ni wa kufanyia kazi, hata kama umetolewa na mtu gani. Kumbuka wewe ndiye mwenye maono na ndoto kubwa za biashara yako, chochote ambacho hakiendani na maono hayo makubwa, hakina nafasi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog