Kwa muda wote ambao nimekuwa najifunza biashara, kupitia mafunzo mbalimbali na hata kufanya biashara, nimekuwa nafananisha biashara na kitu kimoja muhimu; maisha ya mwanadamu. Nashawishika, bila ya shaka yoyote kwamba biashara ina sifa kama ya mwanadamu, kabisa. Biashara zinazaliwa, biashara zinakua, na biashara zinakufa, kama ilivyo kwa binadamu. Ili biashara ziendelee vizuri, zinahitaji kupata matunzo mazuri.
Sasa kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara, hasa wageni, kutaka biashara ianze kufanya maajabu mwanzoni. Yaani biashara imefunguliwa tu basi iwe na wateja wengi, watu wanunue mpaka washindwe kuwahudumia. Inaweza kutokea mara chache na kwa biashara chache. Lakini kwa kawaida, unahitaji muda, watu waione biashara, wapite, waje tena waione, waulizie bei, wapite bila kununua, wapite tena wakuone kisha wajaribu kununua. Ni hali ya kawaida kabisa, watu huamini kitu hadiri wanavyokiona kwa muda mrefu.
Hivyo unapokuwa na biashara mpya, ipe muda biashara yako, ipe muda wa kukua, ipe muda wa watu kuifahamu na ipe muda kabla hujaanza kuitegemea moja kwa moja.
SOMA; Epuka Kosa Hili La Muda Unapoanza Biashara Yako.
Biashara mpya ni kama mtoto mchanga, mtoto yeyote mchanga, miezi sita ya mwanzo ni kipindi muhimu mno kwake, na ndiyo maana inashauriwa anyonyeshwe maziwa tu kwa kipindi hicho. Kwa sababu huo ndiyo wakati ambao uwezekano wake wa kufa ni mkubwa.
Kadhalika, miezi sita ya kwanza ya biashara, ndiyo wakati hatari kabisa kwenye biashara, hapo ndipo penye uwezekano mkubwa wa kufa. Unapaswa kuwa makini sana kwenye kipindi hicho cha biashara.
Hata taasisi za kifedha zinajua hili, nenda kaombe mkopo wa biashara benki na watakuuliza je biashara hiyo ina zaidi ya miezi sita? Kama hapana hawakupi mkopo, kwa sababu wanajua upo kwenye hatari kubwa.
Unapoanza biashara, jipe muda kabla hujakimbia na kusema biashara hailipi, kama ni mwanzoni, jifunze sana na chukua hatua kuboresha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
