Kila ninapokuwa nawauliza watu nini kinawazuia kuingia kwenye biashara, majibu huwa yananishangaza mno. Watu huwa wanataja vitu ambavyo unashangaa vinawezaje kumzuia mtu asiingie kwenye biashara anayotaka kuingia. Watu wengi wamekuwa wakisubiri mpaka wawe kamili kwa kila kitu, mpaka waandae na vipeperushi vya kuwavutia wateja ndiyo waanze biashara rasmi.

Lakini unajua nini, wateja hawanunui vipeperushi, wateja hawanunui teknolojia yoyote mpya ambayo unakuwa umeweka kwenye biashara yako. Mteja anajali teknolojia moja tu kwenye biashara yako; suluhisho la matatizo yake na mahitaji yake. Chochote nje na hapo, hakina mashiko makubwa kwa wateja wako.

Hivyo unapojizuia kuingia kwenye biashara kwa sababu unaona hujawa tayari, kitu ambacho huwa hakitokei, unawanyima wateja haki yao ya msingi kabisa.

Kama una suluhisho ambalo wateja wanalitaka, au una mahitaji ambayo wanayataka, hapo ndiyo sehemu kuu ya kuanzia biashara yako. Hapo ndipo unapaswa kuanza kuwapa wateja kile wanachotaka. Hayo mengine utaendelea kuyaboresha kadiri unavyokwenda.

SOMA; Tengeneza Utegemezi Wa Mteja Kwenye Biashara Yako….

Kitu ambacho watu ambao hawajaingia kwenye biashara hawajajua ni kwamba, mambo mengi unayopanga kabla hujaingia kwenye biashara, huwa yanabadilika ukishaingia kwenye biashara.

Ninachotaka kukuambia hapa ni kwamba, kama unajizuia kuingia kwenye biashara kwa sababu fulani unayoifikiria, sababu hiyo huenda hutaenda nayo kwa muda mrefu kwenye biashara yako.

Hivyo rafiki, kama ambavyo nimekuwa nakuambia, JUST DO IT, yaani anza. Kama unalo suluhisho ambalo watu wanataka, unayo mahitaji ambayo watu wanayatafuta, anza kuwapatia. Mengine utajifunza kadiri unavyokwenda.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog