Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Msingi wetu mkuu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, tupambane sana na msingi huu kwani ndiyo utakaotuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu SUBIRI…
Matatizo mengi kwenye maisha ya watu, yanatokana na watu kukosa uwezo wa KUSUBIRI,
Watu wazima wamejijengea tabia kama ya watoto,
Tabia ya NATAKA KITU NA NINAKITAKA SASA, SITAKI KUSUBIRI HATA KIDOGO.
Hili limewaingiza wengi kwenye matatizo kwa sababu siyo mara zote wanakuwa na uwezo wa kupata kile wanachotaka.
Ila kwa kuwa dunia ipo tayari kuwahadaa, basi inawapa mtego wa kupata kile wanachotaja, lakini mtego ambao utawagharimu baadaye.
Na hapo ndipo watu huingia kwenye vitu kama mikopo, utapeli na njia nyingine zinazowapa kile wanachotaka sasa, kwa gharamanya baadaye.
Ni wakati sasa wa kurudi kwenye msingi, kuondokana na tabia hizi za kitoto.
Badala ya kukimbilia chochote unachotaka, SUBIRI…
Chochote unachojiambia sasa unataka, subiri kwanza,
Hata kama uwezo wa kukipata upo ndani yako, wewe subiri kwanza.
Hii inakuwezesha kujenga nidhamu muhimu kwenye maisha yako, na kuepuka kukazana kupata kile unachotaka, kwa gharama ya baadaye.
Kama kuna kitu unataka kununua, acha kwanza kununua kwa muda kidogo, usikutane tu na kitu na kukimbilia kununua.
Subiri kabla hujakimbilia kufanya maamuzi yoyote.
Japokuwa dunia itakuhadaa kwamba unachelewa, kwamba unakosa fursa nzuri.
Achana na hayo yote, wewe subiri.
Utajifunza mengi mno kwenye kusubiri kuliko kukimbilia kufanya maamuzi.
Katika kusubiri kwako, utakuja kugundua kile ulichokuwa unafikiri unakihitaji sana, kumbe wala haikuwa hivyo, ni hisia tu zilikuwa zinakuendesha wakati huo.
Nirudie rafiki, SUBIRI, huwezi kufa kwa kusubirim labda kama ni jambo la dharura, lakini mengine yote, yasubiri kwanza.
Uwe na siku njema sana leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info