Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana kwetu.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUONEKANA NA WEWE UPO…
Hakuna maamuzi ya hovyo ambayo mtu unaweza kufanya, iwapo tu msukumo wa kufanya ni kuonekana na wewe upo.
Kwa sababu unachofanya kinakuwa siyo sahihi, siyo muhimu na kinakugharimu.
Kwa mfano unaponunua kitu, kwa sababu kila mtu amenunua na wewe unataka kuonekana upo, unaingia gharama ambazo siyo muhimu. Unanunua vitu ambavyo huvijali, na wale unaotaka wakuone na wewe upo pia hawajali sana. Kwa sababu kuda mwingi wapo ‘bize’ na matatizo yao binafsi.
Unapoongea ili tu na wewe uonekane upo, unaishia kuongea kitu cha hovyo, ambacho kitawafanya watu wakutilie shaka kupitia kile ulichoongea. Hata kama utakuwa na kitu kizuri kiasi gani, msukumo ukishakuwa ni kitaka na wewe uonekane, utakiwasilisha vibaya na hapo utatengeneza matatizo zaidi.
Mchekeshaji mmoja amewahi kusema kwamba tatizo la watu ni kwamba wanatumia fedha ambazo hawana, kununua vitu ambavyo hawavipendi ili kuwavutia watu ambao hawajali.
Kauli hiyo ina maana kubwa sana na ukiifanyia kazi, unajiondoa kwenye utumwa mkubwa wa kujitengenezea.
Chochote unachofanya, iwe ni kwa sababu na misingi sahihi, na isiwe ni msukumo wa kutaka kuonekana na wewe upo.
Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info