Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UNAMWANGALIA NANI?
Katika maisha yetu hapa duniani, tunapaswa kuwa na watu ambao tunawaangalia,
Hawa ni watu ambao wamefanya makubwa kwenye kile ambacho sisi tunafanyia kazi.
Watu ambao wameshafika kule ambapo sisi tunataka kufika, na waliofanikiwa kufanya kile ambacho sisi tunataka kufanya.
Watu hawa wanakuwa hamasa kwetu kwamba inawezekana na hivyo hata sisi tunaweza pia.
Watu hawa pia wanakuwa darasa kwetu, kujifunza yale muhimu ya kuzingatia na makosa ya kuepuka katika safari yetu.
Kwa kuwaangalia na kiwafuatilia watu hawa vizuri, njia yetu inakuwa rahisi kidogo kuliko tungekuwa tunajaribu kila kitu sisi wenyewe.
Kwa sababu yapo makosa mengi ambayo wengine wameshayafanya na kujifunza, huna haja ya kuyarudia yote.
Swali muhimu; je unamwangalia nani kwenye safari yako ya mafanikio?
Siyo lazima awe karibu ma wewe, anaweza kuwa mbali kabisa.
Siyo lazima awe anajua unamwangalia, anaweza hata asijue kama upo.
Siyo lazima awe hai, anaweza kuwa alishakufa miaka mingi iloyopita.
Siyo lazima awe mmoja, unaweza kuwa nao wengi utakavyo, ila falsafa zao zisipingane.
Unachohitaji ni kuwa na mtu unayemwangalia, ambaye unaweza kupata taarifa zake, maisha yake na yale makubwa aliyofanya.
Huna haja ya kujaribu kila kitu mwenyewe,
Na hakuna kombe la kujua kila kitu mwenyewe.
Chagua watu ambao utajifunza kwao, na waangalie kwenye safari yako ya maisha ya mafanikio.
Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info