Moja ya sababu inayopelekea biashara nyingi kushindwa kukua na kudumaa, ni wamiliki wa biashara wenyewe. Kwa sababu pale biashara inapokua, mambo yanabadilika, lakini wamiliki wa biashara hizo hawabadiliki. Hivyo wanakuwa kikwazo kwenye ukuaji wa biashara zao.
Kwa mfano kama umeanza biashara na mtaji kidogo, labda wa milioni au chini ya hapo, ukapambana sana mpaka mtaji ukafika milioni 50, kupiga hatua zaidi ya hapo, unahitaji mikakati tofauti na iliyokufikisha hapo.
Mikakati uliyokuwa unatumia wakati mtaji wa biashara ni milioni moja, hautakufaa kama utautumia pale mtaji wa biashara unapokuwa milioni mia moja. Lakini wengi bado wanaendesha biashara zao kama walivyoanza, na watashangaa mbona hawaendi mbele zaidi.
Kwenye kila hatua ya biashara yako, kuna mikakati mipya ambayo unapaswa kuitengeneza, yapo mambo mapya ambayo unapaswa kujifunza.
SOMA; Kushindwa Ni Sehemu Ya Kukua…
Kwa mfano wengi wanapokuwa wanaanza biashara, huwa wanakuwa na mtaji kidogo, hivyo hilo huwapelekea wao kufanya kila kitu. Lakini biashara inapozidi kukua, hawawezi tena kufanya kila kitu, kwa sababu vitu vya kufanya ni vingi. Wanapaswa kuwa mkakati wa kuwawezesha kupata wasaidizi bora wa biashara zao, ambao watawasaidia kukua zaidi. Wengi wanakuwa hawana mkakati huo, hivyo hujikuta wakipata watu wasio sahihi na kupelekea kusumbuka kibiashara.
Biashara inavyozidi kukua, inapaswa kuacha kuendeshwa kama biashara ndogo na kuanza kujengewa mifumo ya kibiashara. Kunapaswa kuwa na vitengo tofauti tofauti vya biashara hiyo ambavyo vinaweza kusimamia maeneo tofauti kwa ukaribu zaidi. Mfano masoko, mauzo, huduma kwa wateja, uzalishaji, rasilimali watu na kadhalika.
Biashara yako inapokua, na wewe unapaswa kukua, tena inabidi ukuaji wako uwe wa kasi kuliko wa biashara, wakati mtaji wa biashara ni milioni kumi, wewe fikiria na panga mikakati ya namna ya kuendesha biashara kwa mtaji wa milioni 100, endelea kwenda hivyo, hatua kubwa mbele zaidi.
Kila unapopiga hatua, weka mikakati mikubwa zaidi. Biashara inapokua, matatizo na changamoto nazo pia zinaongezeka. Hivyo jiandae vizuri kwa hayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
