Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.


Ni kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUTOROKA…
Tofauti ya wale wanaofanya makubwa na wanaoshindwa huwa inaanzia kwenye changamoto wanazokutana nazo.
Kila mtu hukutana na changamoto kwenye safari yake ya mafanikio.
Kile ambacho mtu anafanya anapokutana na changamoto, ndiyo kinapelekea kufanikiwa au kushindwa.

Wanaoshindwa, ambao huwa ni wengi, wanapokutana na changamoto, hukimbilia kutafuta njia ya kutoroka. Huangalia namna gani ya kukwepa changamoto hiyo au kuiondoa kwao.
Hivyo huwa wanapata usumbufu wa kuwaondoa kwenye changamoto kwa kufanya yafuatayo;
1. Kutafuta watu wa kuwalaumu.
2. Kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii.
3. Kufuatilia maisha ya wengine.
4. Kufuatilia habari mbalimbali.
5. Kutumia vilevi.

Lakini kukimbia huku, hakutatui changamoto, bali kunaisogeza mbele tu.
Hivyo baada ya usumbufu huo kuisha, bado hujikita wana changamoto zilezile.

Wale wanaofanikiwa, wanapokutana na changamoto, wanajipa muda wa kuelewa vizuri changamoto ile, kisha kuweka mkakati wa kufanyia kazi. Hupambana kuhakikisha wanavuka changamoto ile na kuweza kufanya makubwa zaidi.
Uzuri wa changamoto ni kwamba, usipotoroka au kuzikimbia, zenyewe zinakimbia, kwa kuwa utaweza kuzitatua.

Hivyo rafiki yangu, unapokutana na changamoto yoyote kwenye maisha yako, na utakutana nazo nyingi, zuia ile hali ya kutaka kutoroka na kutafuta usumbufu. Badala yake tengeneza mpango wa kutatua changamoto ile. Hivi ndivyo mafanikio yanavyotengenezwa.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info