Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.


Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu ASILIMIA MIA MOJA….
Pamoja na kwamba tunaishi kwenye dunia inayoonekana kama haina ukomo wa jambo lolote, hasa kutokana na ukuaji wa teknolojia, tuna ukomo wa vitu vikuu viwili;
1. Muda, tuna masaa 24 pekee kwa siku, hatuwezi kupata zaidi.
2. Nguvu, miili yetu inachoka, huwezi kuwa sawa unapoianza siku na unapoimaliza.

Hivyo kama tupo makini na mafanikio yetu, hizi ndiyo rasilimali tunazopaswa kuzipangilia vizuri sana, kwa sababu ndiyo zinazoweza kutupeleka mbele au kuturudisha nyuma.
Ili kuweza kutumia rasilimali hizi mbili vizuri, kuna sheria moja muhimu sana tunapaswa kufuata, nayo ni sheria ya ASILIMIA MIA MOJA.

Chochote ambacho unafanya kwenye maisha yako, kifanye kwa ASILIMIA MIA MOJA.
Weka nguvu, akili na jitihada zako zote kuhakikisha unakifanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kwa njia hii utaweza kufanya makubwa kwa muda mfupi na nguvu kidogo ulizonazo.

Kama lipo jambo lolote unafanya, ambalo hupo tayari kulifanya kwa asilimia mia moja, basi achana nalo mara moja. Acha kulifanya, acha kabisa. Halina msaada kwako wala kwa yeyote yule. Ni kupoteza muda na nguvu, rasilimali mbili muhimu sana ambazo unazo kwa uhaba.

Usitake kufanya jambo lolote ili tu uonekane unafanya,
Usitake kufanya jambo lolote kuwaridhisha wengine,
Usitake kufanya jambo lolote kwa sababu huna kingine cha kufanya.
Usitake kufanya jambo lolote kwa sababu tu unasukuma muda uende.
Chochote unachofanya, weka kila ulichonacho kuhakikisha unakifanya kwa ubora wa hali ya juu sana.

Kutumia sheria hii ya ASILIMIA MIA MOJA kutakuletea matokeo ya aina mbili;
1. Utaridhishwa na matokeo ambayo utayapata, unapoweka juhudi na kupata matokeo mazuri, unapata hamasa ya kuendelea kufanya zaidi. Utajiona wa thamani na ambaye una mchango mkubwa kupitia kile unachofanya.
2. Utawanufaisha wengine kwa kile unachofanya. Utakuwa na mchango bora owa wengine na wao watakupa kile ambacho unakitaka.

Hivyo rafiki, sehemu ya kuanza kuwa bora, ni hapo ulipo kwa kile unachofanya. Kifanye kwa ASILIMIA MIA MOJA, utapata matokeo bora kabisa kwako na kwa wengine.
Kama kitu huwezi kukifanya kwa asilimia 100, basi achana nacho kabisa, usikifanye, kifute kabisa kwenye maisha yako. Ni matumizi mabaya ya muda na nguvu zako, rasilimali ambazo zipo kwa uhaba mkubwa.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki, kafanye kwa ASILIMIA MIA MOJA.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info