Kama wateja wako siyo watu wa kipato cha chini kabisa, basi msukumo wao wa kununua siyo bei pekee. Watu wa kipato cha chini kabisa, hununua kwa msukumo wa bei pekee. Hivyo kwa kundi hilo la watu, kama ndiyo wateja wako wengi, unahitaji kujiweka vizuri kwenye upande wa bei.

Lakini wateja wako wanapokuwa na uwezo kidogo wa kuchagua, yaani wana uwezo wa kusema nanunua hicho na kuacha kile bila ya kujali sana kuhusu bei, basi msukumo wao mkubwa wa kununua siyo bei, bali mapenzi na kujali.

Watu huwa wapo tayari kulipia kupata kile ambacho wanakipenda kweli. Mtu anapokutana na kitu anachokipenda, atafanya kila juhudi kuhakikisha anakipata, hata kama fedha hana wa wakati huo.

SOMA; Mambo Matano (05) Muhimu Ya Kuzingatia Wakati Wa Kupanga Bei Ya Huduma Au Bidhaa Kwenye Biashara Yako.

Watu watatoa senti yao ya mwisho kupata kile ambacho wanakijali kweli, kile ambacho kinawatatulia changamoto zao, kile ambacho kinatimiza mahitaji yao. Watu wanapokutana na kile wanachojali hasa, hawasiti kuchukua hatua ili wawe nacho.

Hivyo mfanyabiashara, hakikisha kwanza unauza kitu ambacho kina msaada kwa watu, na kazi yako kubwa ni kuwafikia wale watu, wajue uwepo wako, wajue kile ambacho unafanya. Ukishaweza kuwafikia watu sahihi, utaacha kuhangaika na bei na kuanza kuboresha zaidi kile ambacho unawapatia.

Kila bidhaa au huduma ina aina yake ya wateja, wale ambao wanapenda na kujali bidhaa au huduma hiyo. Ni kazi yako kuwafikia hao. Ukishawafikia, kazi yako kubwa ni kuwatatulia changamoto zao, na kuwapa mahitaji yao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog