Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora.


Ni kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UNASIMAMIA NINI?
Iko hivi rafiki, kwenye hii dunia, kama hakuna unachosimamia, kama hakuna unachopigania, kila kitu kitakuangusha.
Maisha hayajawahi kuwa rahisi wala hayatakuja kuwa rahisi,
Dunia siyo fair na wala hakuna aliyekuahidi kwamba itakuja kuwa fair,
Kwanza dunia haijali kwamba upo au haupo, ulikuja ukaikuta, na utaondoka na kuiacha.
Dunia inaongozwa kwa sheria za asili, ambazo hazina huruma kwa yeyote yule, hasa anayezivunja.
Kwa mfano simba wataendelea kuwala swala, hata kama swala watatalalamika kiasi gani.
Na pia katika simba kumla swala, swala dhaifu wataanza kuliwa kabla ya swala imara.
Dunia haipendi vitu dhaifu, kuanzia kwa wanyama, mimea na hata binadamu.
Vitu dhaifu vinateswa, viu dhaifu vinaliwa, viti dhaifu vinapotezwa.

Na hii ndiyo maana asubuhi ya leo ni muhimu kutafakari unasimamia nini kwenye hii dunia. Kwa sababu kama hakuna unachosimamia, utaishia kuliwa, utaishia kutumiwa na wengine, utaishia kuteseka na kuona maisha hayafai.
Kama hakuna ndoto zako kubwa unazopigania, utaishia kupigania ndoto za wengine, dunia haitakuwa na huruma na wewe.
Kama huna misingi ambayo unaisimamia kwenye maisha yako, utashurutishwa na wengine kusimamia misingi yao.

Hivyo ndivyo hali ilivyo rafiki,
Ndiyo uhalisia wa dunia,
Lazima uwe imara,
Lazima uchague unasimamia na kupigania nini,
Lazima uwe na misingi ambayo unaisimamia kwenye maisha yako.
Lazima uwe na nidhamu ya hali ya juu, kwako wewe binafsi.

Tofauti na hapo utaliwa,
Tofauti na hapo utaangushwa,
Tofauti na hapo utatumika kufanyia kazi ndoto za wengine,
Tofauti na hapo utaishia kulalamika dunia haipo fair.

Swali muhimu kujiuliza ni unasimamia nini na umejitoa kiasi gani, upo tayari kupambana kiasi gani. Na dunia itakupa kile unachotaka, kutokana na namna unavyosimama na kupambana. Ukikosa hivyo, dunia itakufanya kuwa chakula au matumizi ya wale ambao wamechagua kusimama na kupambana.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki, uende ukasimamie kila unachotaka, uende kufanya makubwa na kwa ubora zaidi.

Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info