Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. 



Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza madhara ya kuwa na njaa ya aina yoyote katika maisha yako.

Dunia ya leo watu wenye njaa ndiyo wanaosumbuliwa sana na kuteseka. Kuna njaa nyingi sana ambazo watu wengi wanasumbuliwa nazo ni njaa katika nyanja mbalimbali katika maisha yetu. Inaweza kuwa njaa ya kiroho, kimwili na kiakili. Watu wanaumwa na njaa na matokeo yake njaa inawafanya wapate kile kitu ambacho hakistahili.

Ndugu msomaji, kitu kikubwa cha kukiepuka katika maisha yako basi ni njaa yoyote ile kwa sababu mtu mwenye njaa huweza kula kitu chochote kile ili aweze kushiba tu. 

Tunaalikwa kuepuka kuwa na njaa katika maisha yetu hapa ninazungumzia njaa yoyote ile kwa sababu kila mtu ana njaa yake.

Madhara ya kutanguliza njaa wenye kitu chochote kile ni shida kubwa. Kwa mfano watu ambao wana njaa ya mafanikio wanakuwa ni rahisi kutapeliwa kwa sababu wanakuwa na njaa ya kupata mafanikio ya haraka bila kufanya kazi. Wanataka mafanikio ya haraka kama vile hayaji hivyo mtu ambaye anakuwa na njaa kama hii inampelekea kutumiwa vibaya na njaa yake.

Rafiki, dunia ya leo usipokuwa makini utaumia sana wale watu ambao wanaonesha wana njaa ya kitu fulani huwa wanatumia vibaya sana. Hata wale wanaokwenda kuomba kazi na kuambiwa mshahara mdogo kabisa hawezi kukataa kwa sababu tayari ameshaonesha njaa yake juu ya kitu hicho. Watu wanatumia njaa yako kukuchapia au kukuumiza bila ya wewe kujua.

Kuna wale watu ambao wanakuwa na njaa ya kiroho sasa na ubaya wake watu ambao wanakuwa na njaa ya kiroho wanakuwa hawajui ukweli. Hivyo kulingana na njaa yao ndiyo maana ni rahisi kutekeka, utawasikia watu wengi siku hizi wanaanzisha nyumba zao za ibada na kuanza kuhubiri injili ya mafanikio. Watu wanatumia njaa ya watu kuwapiga kabisa, watu wa leo ni wajanja wanajua kabisa dunia ina njaa ya kiuchumi, mahusiano na nk hivyo wanaambiwa njoo tukuombee na matatizo yako yatapona na utafanikiwa.

Shida ya watu ni kuwa ukishajua njaa yao ni rahisi kuwateka. Wengine njaa yao ni ujinga sasa mtu ambaye ni mjinga na hapendi kujifunza anapenda tu kusikia kitu kutoka kwa watu bila ya yeye mwenyewe kukaa chini na kujifunza ni rahisi kukamatika. Njaa ya ujinga inawakamata watu wengi na hatimaye kurubuniwa. Watu hawapendi kusoma na wala kujifunza kwa watu waliofanikiwa. Leo hii watu wanapenda tu vitu vya bure ukimwambia mtu achangie gharama hataki ndiyo anakimbia kabisa.

Mpenzi msomaji, njaa ya dunia ni kubwa sana na ndiyo ujinga wa leo. Watu wanapenda kupokea tu bila kutoa wanasahau kabisa kuhusu sheria ya asili jinsi ilivyo. Dunia ina njaa nyingi na siwezi kuandika hapa njaa zote. Kuna watu wengine wana njaa ya mapenzi hivyo njaa ya mapenzi inawapelekea hata muda mwingine kubaka na kuongozwa na hisia katika kutafuta mweza hatimaye kupata mtu ambaye siyo sahihi katika maisha yake.

Hatua ya kuchukua leo, kiafya tunashauriwa tuepuke kuwa na njaa kwa sababu njaa itakupelekea hata kula chakula cha hovyo kabisa. Matokeo ya kula chakula cha hovyo ni kuharibu afya yako. Epuka njaa ya aina yoyote ile kwani njaa itakupelekea kutumiwa vibaya.

Kwa hiyo, kila mtu ana njaa yake hapa duniani. Ila usikubali kabisa uendeshwe na hisia kubwa ya njaa na ukishaonesha njaa yako ni rahisi watu kukuumiza na njaa yako. 

Unatakiwa kuwa mgumu na kutulia lakini pia kujikaza kwa ndani huku ukiwa unasoma mchezo taratibu. Ukionesha wewe ndiyo una njaa sana ya kutaka mafanikio ya kifedha kwa haraka ni rahisi kutapeliwa na kulizwa. Usipende kabisa vitu vya bure katika maisha yako au vitu rahisi kwa sababu vitakuumiza na ukiongeza na njaa ya kitu fulani. Njaa ni mbaya ya kitu chochote kile kwa sababu itakusababishia kufanya kitu cha ajabu.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi. Asante sana.