Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UNAKUWA UNACHOFIKIRI….
Moja ya ugunduzi mkubwa uliowahi kufanyika kwenye saikolojia ya binadamu na sayansi ya mafanikio ni kwamba mtu yupo pale alipo kwa sababu ya fikra ambazo ameruhusu kutawala akili yake.
Kwa kifupi ni kwamba unakuwa kile unachofikiri, matokeo yako ya nje, ni zao la fikra za akili yako.
Wengi wanajua hili, lakini wanalijua nusu.
Wanachojua ni kwamba ukiwa na mawazo chanya basi utapata vitu chanya na maisha yako kuwa vizuri. Wanakazana kuwa na mawazo chanya lakini maisha yao yanazidi kuwa magumu.
Ukwei unaopaswa kuujua kuhusu dhana hii ya UNAKUWA UNACHOFIKIRI ni kwamba, sehemu ya akili yako yenye nguvu kubwa(subconscious mind), haitambui mawazo chanya wala hasi, yenyewe inachukua kila wazo na kulifanyia kazi. Na yale mawazo au fikra zinazojirudia mara kwa mara ndiyo zinazotekelezwa.
Hii ina maana kwamba kile unachofikiri kwa muda mrefu, iwe unajua au hujui, ndiyo kinachotokea kwenye maisha yako, na siyo tu kile unachochagua kufikiri kwa muda fulani.
Kwa mfano, kama kuna kitu hukipendi, maana yake unaruhusu akili yako iwe na fikra juu ya kit hicho, na cha kushangaza kila mara utaendelea kukipata, japo hukipendi. Hata kama kuna muda utajilazimisha kuwa na fikra chanya, mwisho wa siku utaendelea kupata au kuona kile ambacho una chuki nacho.
Kadhalika kama kuna kitu unataka lakini ukajiambia huwezi kupata, kweli hutakipata.
Au ukaiambia mtu fulani ana dharau, kila neno litakalotoka mdomoni kwake litakuwa la dharau.
Au ukajiambia kila wakati unakutana na matatizo, kila wakati utakutana na matatizo.
Au ukajiambia wewe huthaminiwi, hata mtoto mdogo hatakuthamini.
Kitu kikibwa ambacho watu wengi hatujui ni kwamba sehemu hii ya akili ambayo ina nguvu sana (subconscious mind), inafanya kazi kwa kutumia picha na siyo fikra. Sasa unapofikiri jambo lolote, unatuma picha ya jambo hilo kwenye sehemu yako ya akili, na yenyewe inafanya kazi kuhakikisha picha ile inatokea kama vile unavyoifikiria, na mara nyingi mno, unapata picha kama ulivyokuwa unafikiria…
Halfu unajiambia NILIJUA TU!! Kama vile ni maajabu makubwa sana.
Nisisitize tu ya kwamba, hupati matokeo mazuri kwa kuwa na dakika chache za siku ambapo unakuwa na fikra nzuri. Bali unapata matokeo yanayotokana na zile fikra zinazotawala akili yako kwa muda mrefu.
Kwa mfano kama unajipa dakika kadhaa za kufikiri chanya, halafu unatoka hapo unaenda kukaa na watu wanaozungumzia namna gani mambo ni mabaya,
Unatoka hapo na kwenda kusikiliza redio ambayo inaeleza namba gani mambo ni mabaya,
Unafungulia TV nayo mambo ni mabaya,
Unachukua gazeti napo msisitizo ni kwamba mambo ni mabaya,
Ukichomoka hapo na kupata matokeo mazuri, utakuwa mwenye bahati sana, japo bahati haipo.
Hii ni kwa sababu akili yako inakuwa imechafuliwa na kutawaliwa na fikra kwamba mambo ni mabaya.
Ni wakati sasa wa kutawala fikra zako kwa mawazo na fikra chanya, kubwa na za uwezekano.
Ni wakati sasa wa kulinda akili yako, kuhakikisha haichafuliwi na mawazo na hofu za watu wengine.
Ni wakati wa kuamua ufikiri nini kwa masaa 24 ya siku yako.
Ni wakati wa kuachana na hofu zote zinazokuzuia,
Ni wakati wa kuondokana na kila aina ya chuki uliyonayo.
Ni wakati pia wa kusamehe, ili fikra zako ziwe safi na utengeneze matokeo bora sana kwako.
Unaonaje, leo si utakiwa na siku bora sana? Itakuwa kama utataka iwe.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info