MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo makubwa.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa sana siku ya leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu HAPO ULIPO SASA…
Hapo ulipo sasa, kunaweza kuwa adui mkubwa wa kule unakotaka kwenda.
Kwa sababu kama unafurahia hapo ulipo sasa, hutapata hasira ya kubadilika.
Kama umeridhika na hapo ulipo sasa, utaendelea kuwa hapo hapo miaka yako yote.
Kama umeshazoea hapo ulipo sasa, na kuona hiyo ndiyo njia pekee iliyopo, utaendelea kuwa hapo hapo miaka yako yote.
Hivyo rafiki yangu, asubuhi hii tafakari je hapo ulipo sasa, ndipo unapotaka kuwepo kwa maisha yako yote?
Je umekuwa hapo kwa muda gani?
Je kipi kinakusukuma usiendelee kuwepo hapo ulipo sasa?
Ni kawaida yetu binadamu kuzoea kitu halafu kutengeneza maisha yetu kuendana na kile ambacho tumezoea.
Kubadilika, lazima uanze kubadili yale ambayo umeyazoea, ndiyo uweze kupiga hatua.
Kataa hapo ulipo sasa, kama unataka kufika mbali zaidi ya hapo. Ukishapakataa, tengeneza mkakati wa kukutoa hapo ulipo.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.