MAKIRITA AMANI:

Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambao utatuwezesha kufanya makubwa kwenye maisha yetu na kufanikiwa.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu CONSISTENCY…

Hakuna kitu ambacho unaweza kufanya mara moja kwenye maisha yako na kikakuletea mafanikio makubwa.

Mafanikio yoyote, yanatokana na kuchagua aina ya maisha ya mafanikio unayotaka, na kuyaishi hayo siku zote.

Lazima uwe thabiti, kurudia kitu mara kwa mara ndiyo uweze kuona matokeo mazuri na makubwa.

Ni rahisi kuanza kitu kipya, kwa sababu huwa kunakuwa na hamasa mwanzoni. Lakini baada ya muda, changamoto huwa zinajitokeza, na ile hamasa ya mwanzo kuondoka. Hapa ndipo wengi huacha kufanya na kutafuta kingine cha kufanya.

Wanaofanikiwa, huendelea kufanya licha ya hamasa kuisha na changamoto kuwepo. Ni kuendelea kwao kufanya ndiyo kunawapa manufaa makubwa, kwa sababu wanakuwa wamebaki wachache na wengi wanakuwa wameshaacha.

Chochote unachofanya rafiki, hakikisha unaweza kukifanya kwa muda mrefu. Hakikisha unajiandaa kukifanya kila siku kwa siku nyingi sana zijazo.

Kinachoifanya dunia iendelee kuwepo ni CONSSTENCY, dunia inazunguka jua, na mwezi unazunguka dunia. Tunapata usiku na mchana na tunapata majira ya mwaka, kila mwaka.

Ukiweza kuchagua kufanya kile unachofanya vizuri, na kuendelea kukifanya kila siku kwa viwango, dunia itakuwa tayari kukupa kile ambacho unataka.

Changamoto kwa wengi ni kutaka matokeo ya haraka, na wasipoyapata wanaachana na kile wanachofanya na kutafuta kingine cha kufanya.

Utahangaika na kutafuta mengi, lakini kama hutachagua kitu kimoja au vichache ambavyo unaweza kuvifanya kwa muda mrefu, utakuwa unaishi maisha ya kuendelea kujaribu kila wakati, bila ya mafanikio yoyote.

Chagua kile unataka kufanya, na kifanye kila siku kwa muda mrefu, hili ni hitaji muhimu mno la mafanikio.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

http://www.makirita.info