MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UMEKAMILIKA JINSI ULIVYO…
Watu wengi wamekuwa wana mipango mikubwa sana ya maisha ya mafanikio.
Lakini inapokuja kwenye utekelezaji, kwenye kuanza kuchukua hatua, hujishawishi kwamba bado hawajakamilika.
Hapa hujiambia nikishapata kitu fulani, basi nitaweza kuanza vizuri, au nikimaliza kitu fulani ndiyo nitaweza kuanza.
Ukweli ni kwamba, kwa jambo lolote kubwa na muhimu sana kwako, kama huwezi kuanza kulifanya sasa, hutakuja kuweza kulifanya.
Kwa sababu hakuna wakati wowote kwenye maisha yako ambapo utajiona umeshakamilika na upo tayari kufanya.
Kila wakati utaona kuna kitu bado hujakamilisha, utaona kuna kitu umekosa.
Ukweli ni kwamba, unaweza kuanzia hapo ulipo sasa, ukifanya hayo unayoweza kufanya sasa, huku ukikua kadiri unavyokwenda.
Usiendelee kujidanganya kwamba kuna wakati utakuwa kamili zaidi ya ulivyo sasa. Hakuna wakati kama huo, hivyo ni vyema mno kama utaanza SASA.
Kwa jambo lolote unalotaka kufanya, ipo sehemu unayoweza kuanzia, ukiwa hapo ulipo sasa na kwa mazingira uliyonayo sasa.
Je unaanzia wapi kwenye hilo ambalo umekuwa unaliahirisha kila wakati?
Anza leo au jiambie wazi kwamba hutakuja kufanya tena.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.