Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo, nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MNYAMA HATARI sana, ambaye akishatoroka kwenye kizimba chake ni vigumu sana kumrudisha.
Mnyama huyu ni hatari na anaweza kuvunja kila kitu ambacho mtu ametengeneza kwa muda mrefu.
Mnyama huyu anaunguza kama moto wa msituni, ambao ukishaanza kuwaka ni vigumu sana kuudhibiti.
Mnyama huyu kila mmoja wetu anamiliki, na hivyo tunatembea na hatari ya mnyama huyu kututoroka na kuleta madhara haya makubwa.
Mnyama tunayemzungumzia hapa ni ULIMI…
Ulimi ni mnyama hatari sana ambaye kama utashindwa kumdhibiti, atakuletea madhara makubwa sana.
Atakuingiza kwenye matatizo makubwa pale unaposhindwa kumdhibiti.
Pia anaweza kuvunja mahusiano ya kila aina.
Kuwa makini sana na ulimi wako,
Fikiria kabla hujaongea na usiwe kama wengi ambao huongea kwanza halafu ndiyo wanafikiria.
Tumia muda mwingi kusikiliza na kuangalia kuliko kuongea. Una macho mawili na masikio mawili, lakini mdomo mmoja. Tumia macho na masikio mara mbili ya unavyotumia mdomo.
Muhimu kabisa kumbuka mjinga akikaa kimya anaweza kudhaniwa ni mtu mwerevu, lakini akiwa mtu wa kuongea ongea, ujinga wake unakuwa dhahiri kwa kila mtu.
Na pia kadiri unavyoongea sana, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kuongea neno la kijinga.
Dhibiti sana ulimi wako, sema kile ambacho ni muhimu kusema kisha kaa kimya, sikiliza na angalia. Siyo lazima usemee kila kitu, siyo lazima ujibu kila kitu na siyo lazima utoe maoni yako kwenye kila jambo.
Kukaa kimya kutakuepusha na matatizo mengi sana kwenye maisha yako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.