MAKIRITA AMANI:
Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, ni siku mpya ya wiki mpya ambapo tunapata nafasi nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye yale ambayo tumechagua kufanya. Kwa juhudi kubwa tunazokwenda kuweka, tuna uhakika wa kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambao unatuwezesha kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu DUNIA SIYO FAIR…
Hii ni kauli ambayo imekuwa inatumiwa na wengi, katika kulalamikia namna ambavyo dunia inakwenda.
Unakuta mtu amefanya kila anachopaswa kufanya, lakini anapata matokeo tofauti kabisa na alivyotegemea.
Au anaweka juhudi yeye, lakini mtu mwingine ndiyo anakuja kubeba pongezi.
Au yeye anaweka juhudi kubwa, halafu anaondolewa au kushindwa wakati ambaye alikuwa haweki juhudi anapata nafasi nzuri.
Hapa ndipo mtu anashawishika kusema kwamba dunia haipo fair, kwamba dunia ina upendeleo kwa watu fulani fulani.
Ukweli ni kwamba dunia ipo fair sana, tena kupitiliza.
Kitendo cha wewe kuwa hai mpaka leo, ni dunia kuwa fair sana kwako, kwa sababu wapo waliokufa kwa matetemeko, mafuriko, na majanga mengine, yote hayo yanatokea hapa hapa duniani, kwa nini hayajakuondoa wewe?
Kwa vipimo vyovyote vile, wapo watu ambao maisha yao ni magumu mno kuliko yako, labda hawana macho, au hawana viungo vyote vya mwili, lakini wanasukuma maisha. Sasa wewe unapata wapi hiyo courage ya kusema dunia haipo fair kwa sababu tu kuna kitu kimekwama?
Dunia inafanya yake, haijali kama upo au haupo. Hivyo kusema dunia haipo fair, unakuwa huitendei haki dunia. Kwa sababu ulikuja ukaikuta, na utaondoka na kuiacha.
Badala ya kukazana kuangalia nini dunia imekunyima, hebu anza kuangalia nini dunia imekupa, ambavyo watu wengine hawana. Halafu jifunze kuwa na shukrani kwa kila jambo, na kuangalia namna gani unaweza kusonga mbele zaidi licha ya kukutana na changamoto.
Kama dunia haipo fair, ni kwa sababu inakupendelea wewe, ndiyo maana mpaka sasa upo hai. Tumia nafasi hii kufanya mazuri ili uweze kufika kule unakotaka kufika.
KUTHUBUTU
USHINDI
SHUKRANI.
Hizi ni kauli tatu zinazotuongoza mwaka huu.
Nenda kathubutu kufanya kitu leo, kitu ambacho hujawahi kufanya au una hofu ya kufanya.
Kapate ushindi leo, hata kama ni mdogo sana, hakikisha kuna kitu unashinda.
Kisha shukuru kwa siku hii, shukuru kwa kila unalopitia, liwe zuri au baya, ni sehemu ya maisha na sehemu ya kujifunza kuwa bora zaidi hapa duniani.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.