MAKIRITA AMANI:

Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?

Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu ambapo tumepata nafasi nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo makubwa.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tunatafakari kuhusu HUJACHELEWA ILA UNAJICHELEWESHA…

Ni mara ngapi kwenye maisha yako umewahi kukutana na jambo kubwa na zuri ambalo ulikuwa hulijui?

Jambo hilo linakushangaza sana, na unaona kwa nini hukuwa umelijua wakati wote huo?

Hapo unaona kama umechelewa sana, na kujilaumu kwa nini umechelewa kiasi hicho.

Lakini nini kinatokea baada ya kujua kwamba umechelewa kujua lile ambalo umejua sasa?

Wengi wamekuwa hawachukui hatua yoyote.

Wengi hukata tamaa zaidi, na kuona muda umeshawapita. Hujiambia kama wangejua mapema basi ingewasaidia. Hivyo wanarudi kuendelea na maisha yao.

Jambo lolote ambalo hujalijua, ukilijua sasa, basi hujachelewa. Ni kwamba wakati wako wa kulijua ulikuwa bado, hivyo unapojua jambo lolote, jua wakati wako ndiyo umefika na wala hujachelewa.

Tatizo kubwa linakuja pale ambapo umeshajua jambo, halafu hakuna hatua unazochukua. Hapa ndiyo unajichelewesha. Umeshajua unapaswa kufanya nini ila hufanyi! Hapo unakuwa unategemea nini?

Kwenye maisha ya mafanikio, hakuna kuchelewa. Wapo wengi ambao wamebadili maisha yao wakiwa na umri mkubwa kabisa na kuweza kuishi maisha ya ndoto zao.

Kwenye maisha ya mafanikio kuna kujichelewesha, pale ambapo mtu unajua nini unapaswa kufanya lakini hufanyi. Kwa sababu yoyote unayojipa ni uongo, unajifariji pekee, kama unajua na hufanyi, umechagua kujichelewesha.

Na wewe unayejua halafu hufanyi, unaumia zaidi kuliko yule ambaye hajui kabisa.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

http://www.makirita.info