Mojawapo ya changamoto kubwa iliyo kwa wengi ni changamoto inayohusiana na mambo ya fedha. Linapotajwa eneo la fedha kwa wengi imekuwa ni changamoto sana na hii ni kutokana na misingi mibovu ya pesa au kukosa elimu ya fedha kabisa.
Kama ambavyo tumekuwa tukiona kupitia masomo mbalimbali hapa AMKA MTANZANIA ama kwenye mtandao mama KISIMA CHA MAARIFA, ili kuwa na fedha za kudumu maishani mwako unahitaji kutengeneza msingi imara sana.
Bila kuwa na msingi imara hautaweza kuwa na pesa za kudumu sana, zaidi utaendelea kuwa mtu ambaye leo una pesa lakini kesho hauna, yaani kwa kifupi unakuwa ni mtu ambaye hutabiriki kipesa kitu ambacho sio kizuri.
Mbaya zaidi umekuwa ni mtu wa kulaumu na kulalamikia kila hali, nakujiona kama umeonewa kutokana na hali unayopitia. Hiyo haitoshi hata akili yako umekuwa ukiaminisha kwamba matatizo ya kifedha kwako ni kama halali yako.
Imefika mahali tatizo la kukosa pesa limekuwa likikukera sana na kushindwa kujua ufanye ili kuondokana na hali hiyo. Leo kupitia makala haya nakupa njia mbadala zingine, kama tatizo lako ni kukosa pesa kila wakati, nini kingine cha kufanya.

1. Tafuta mtu wa kukubadilisha mawazo yako.
Umekuwa ukiendelea kubaki hapo kila wakati na kuzama kwenye changamoto za kifedha kwa sababu ya akili zako. Chanzo cha kukwama ni kwa sababu umekuwa na akili ambazo ziko palepale au akili mgando kwa lugha nyingine.
Ili uweze kufanikiwa na kutoka hapo unatakiwa umpate mtu wa kukuongoza katika eneo la kifedha. Mtu huyu wa kukuongoza anatakiwa awe ndiye kocha wako. Haijalishi utamlipa pesa kiasi gani lakini kama atakusaidia kukupa tiba ya kipesa, lipa pesa hizo mara moja.
Acha kuendelea kujifanya mjuaji, wajuaji wote hawafanikiwi sana katika maisha yao. Wajuaji wanaendelea kubaki pale pale kwenye maisha yako kwa sababu hakuna wanachojifunza cha maana kutoka kwa wengine. Tafuta mtu wa kukubadilisha mawazo yako, utafanikiwa.
2. Usiogope tena kuwekeza.
Tayari ulipo una hali ngumu kifedha na hali inazidi kuwa mbaya siku zinavyozidi kwenda mbele. Siri pekee ya kuweza kuondokana na hali uliyonayo ni kuwekeza. Huhitaji kuogopa kitu kwenye kuwekeza.
Anza kuwekeza kwenye kile kidogo ulichonacho ili kikusaidie kuweza kupata kikubwa. Lakini ukibaki unaogopa kuwekeza basi utaendelea kubaki na maisha yako yaleyale. Asikutishie mtu au kisikutishe chochote, anza kuwekeza mara moja ili kubadilisha maisha yako.
3. Tatizo la kukosa pesa sio lako tu, tafuta njia.
Elewa pia wakati unalalamika na hali yako ngumu, tatizo la kukosa pesa sio lako peke yako. Hivyo hutakiwi kujiona mnyonge sana zaidi unatakiwa kuzidi kuwekeza juhudi kubwa  za kukutoa hapo.
Ukiweka juhudi na kukubali kukabiliana na changamoto inayokukabili, utashinda tatizo la fedha linalokukabili. Amua kufanya kazi kwa nguvu zote na ujitume, utabadilisha maisha yako sana.
Nakutakia siku njema na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,