MAKIRITA AMANI:

Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?

Ni siku nyingine nzuri sana leo ambapo tumepata nafasi nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MUDA UNAO…

Kisingizio cha wengi kwenye kushindwa kufanya makubwa kwenye maisha yao ni kukosa muda.

Lakini tuwe wakweli, hakuna muda zaidi ya masaa 24 ambayo kila mtu anayo kila siku, siku saba za wiki na siku 365 kwa mwaka.

Wote tuna muda huo huo, lakini wapo wanaoutumia vizuri na kufanya makubwa, na wengine wanashangaa hivi muda umeenda wapi!

Ninachokuambia rafiki ni kwamba muda unao, tena wa kutosha sana. Ila tu umeshindwa kupangilia muda wako vizuri, umeshindwa kuweka vipaumbele vyako sawa.

Kama kuna kitu unataka kufanya lakini unasema huna muda, jiulize je kitu hicho ni muhimu hasa?

Kama kitu hicho ni muhimu kweli, jiulize je ni kitu gani unafanya sasa ambacho siyo muhimu kama kile unachotaka kufanya. Halafu acha hicho unachofanya sasa na kufanya kile ambacho ni muhimu kwako.

Kinachowaponza wengi ni kutaka mabadiliko yatokee lakini waendelee kuishi vile vile. Yaani unataka kupata muda wa kufanya mambo muhimu na makubwa kwako, lakini hutaki kuacha chochote unachofanya sasa. Hayo yatakuwa maajabu, labda kama una njia ya kupata masaa zaidi ya 24 kwa siku. Ila kama huna, lazima uchague kuacha vitu fulani, tena vizuri, ili uweze kupata vitu bora zaidi.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

http://www.makirita.info