Nikupe siri moja muhimu kuhusu biashara, haipo biashara ambayo utaweza kufanya wewe pekee hapa duniani. Hata kama utajiwekea hatimiliki ya wazo lako la biashara, watu watabadili kidogo na kufanya kama wanavyotaka wao wenyewe.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanapoteza muda na rasilimali nyingi kuangalia washindani wa kibiashara wanafanya nini kuliko wanavyotumia kwenye kuwahudumia wateja wao.

Tatizo moja ni kwamba, pale unapoweka muda wako mwingi kwa washindani wako, unasukumwa kushindana nao. Na ukishaanza kushindana na yeyote moja kwa moja, unapoteza wateja, lazima.

Hivyo kitu muhimu sana kwa kila mfanyabiashara kufanya siyo kuangalia washindani wanafanya nini na kushindana, bali kuangalia wateja wanahitaji nini na kuwapatia.

Siri ya wazi kuhusu wateja ni kwamba, hawajali wewe unamzidi mshindani wako kiasi gani, wanachojali ni mahitaji na matatizo yao yanatatuliwa wapi vizuri.

Hivyo wakati wewe unakazana kushindana, mteja wako anakazana kutafuta suluhisho la changamoto zake na wapi wa kutimiza mahitaji yake.

SOMA; Ushindi Wa Wengine Ni Muhimu Kwetu…

Unaweza kuangalia washindani wanafanya nini, kwa lengo la kujifunza, lakini kazi yako kubwa ni kuwahudumia wateja wako vizuri, kuhakikisha unawawezesha kutatua changamoto zao na kuwapa mahitaji yao.

Kumbuka siyo wewe wala washindani wako wa kibiashara atakayedumu muda mrefu kama hamtakuwa bora zaidi kulingana na mahitaji ya wateja. Hivyo nguvu yoyote unayotaka kuweka kwenye kushindana, ipeleke kwenye kuwa bora zaidi katika kuwahudumia wateja wako. Na hii itakulipa sana kibiashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog