MAKIRITA AMANI:
Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera sana kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUWAPA RUHUSA WENGINE…
Kuna wakati huwa tunafikiri kwamba dunia inapaswa kwenda kama tunavyotaka sisi.
Kwamba kila tulichopanga basi kitokee kama tulivyopanga.
Huku ni kujidanganya kwa hali ya juu.
Katika kujidanganya huku pia, tumekuwa tunataka watu wawe kama tunavyotaka sisi.
Wawe na tabia zile tunazotaka na wafanye yale ambayo sisi tunataka.
Pia hatutaki kabisa watu wengine wakosee,
Hili limekuwa linaharibu mahusiano mengi ya watu, na mahusiano ya aina yoyote ile.
Kila mtu ana ndoto zake, ana mipango yake na mara nyingi haitafanana kabisa na yako.
Kila mtu ana matatizo yake, changamoto zake na mapungufu yake ambavyo vitampelekea afanye tofauti na ulivyotaka wewe.
Hivyo njia bora kabisa ya wewe kuendelea vizuri na maisha yako na wengine nao kuendelea vizuri na maisha yao, ni kuwapa ruhusa.
Wape watu ruhusa ya kuwa vile walivyo,
Wape watu ruhusa ya kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwao,
Wape watu ruhusa ya kukosea.
Acha kabisa kutaka kuwa kiranja wa dunia nzima, na maisha ya kila mtu yatakwenda vizuri.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.