Pamoja na ushauri mzuri wa kibiashara unaoweza kuupata kutoka kwa watu wengine, lipo jambo moja muhimu sana unalopaswa kujua, biashara yako ni tofauti na ya kipekee.

Unaweza kupewa ushauri mzuri na bora kabisa wa biashara, ukautumia kama ulivyopewa na bado biashara yako ikashindwa.

Tatizo kubwa ni kwamba wafanyabiashara wengi ni wavivu kwenye kufanyia kazi ushauri wa biashara wanaopewa. Wao wakishapewa ushauri, wanaufanyia kazi kama ulivyo, hawaboreshi chochote, halafu wanashangaa kwa nini hawapati matokeo mazuri.

Kama nilivyosema, biashara yako ni ya tofauti, biashara yako ni ya kipekee na huenda wewe pekee ndiye unayeielewa biashara yako zaidi ya mtu mwingine yeyote.

Hivyo basi, unapopewa ushauri wowote wa biashara, usiwe mvivu kwa kuufanyia kazi kama ulivyo, badala yake kaa chini na iangalie biashara yako kwa undani, kisha jiulize kila ulichoshauriwa unawezaje kukitumia kwenye biashara yako?

Jiulize ni kwa namna gani unaweza kukiweka kile ulichoshauriwa au kujifunza kwenye biashara yako, kulingana na unavyoifahamu biashara yako na pia mazingira yako.

SOMA; BIASHARA LEO; Kabla Hujafanya Maamuzi Kutokana Na Maoni Ya Watu, Fikiria Hili…

Kwa njia hii, utaona namna bora kabisa ya kutumia ushauri au mafunzo ya kibiashara unayopata katika kufanikiwa kwenye biashara.

Hakuna ushauri mmoja ambao unaweza kufanya kazi kwenye kila aina ya biashara. Na hata wengi ambao unaweza kuona wamefanikiwa kwenye biashara, wengi hawaelewi kipi kimoja ambacho kimewaletea mafanikio makubwa.

Kadiri unavyoielewa biashara yako na kuzidi kuiboresha ndivyo unavyozidi kufanikiwa.

Kushauriwa kitu na kukichukua kama kilivyo haina tofauti na mtu aliyeibia majibu kwenye mtihani, lakini akanakili mpaka jina la mwenzake, hata kama majibu ni sahihi, atafeli mtihani ule.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog