Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, ambapo tumepata nafasi ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa na kupata matokeo bora sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MUDA MZURI NI KABLA….
Muda mzuri wa kusoma kwa ajili ya mtihani ni kabla ya mtihani.
Muda mzuri wa kuboresha mahusiano yako na wengine ni kabla mahusiano hayo hayajavunjika.
Muda mzuri wa kulinda afya yako ni kabla ugonjwa haujaingia.
Muda mzuri wa kumbakisha mteja kwenye biashara yako, ni kabla hajaondoka.
Muda mzuri wa kufanya kampeni ni kabla ya uchaguzi.
Kabla ya kitu kutokea, tuna nafasi kubwa sana ya kukiboresha kitu hicho,
Lakini sasa, huwa tunazoea vitu, huwa tunafanya kwa mazoea, huwa tunaona vitu vipo na muda upo.
Kwa kufikiri muda upo na vitu vipo, tunapoteza nafasi ya kuvifanya kuwa bora zaidi.
Ni pale vitu vinapokwenda tofauti, ndipo tunastuka na kuanza kuhangaika kubadili. Wakati huo mambo yanakuwa magumu na hatuwezi kuyarudisha kama yalivyokuwa awali.
Muda mzuri ni kabla, asubuhi hii hebu tafakari ni vitu gani unavichukulia kwa mazoea kwenye maisha yako, ambavyo hufanyi juhudi za makusudi kuviboresha zaidi? Kisha anza kuvifanyia kazi leo na kila siku.
Chochote kile ambacho ni muhimu kwako, una nafasi ya kukifanya bora sasa kabla hakijaingia kwenye matatizo.
Je utafanya hivyo leo?
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.