Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MAANDALIZI YA KUISHI au KUJIANDAA KUISHI…
Je kwa sasa kipo kitu chochote ambacho unafikiri ukishakikamilisha au kukimaliza ndiyo utaanza kuishi?
Labda upo masomoni na unaona ukishamaliza masomo basi ndiyo maisha yataanza?
Au upo kwenye ajira ambayo huitaki na unafikiri ukishapata ajira unayotaka ndiyo maisha yataanza?
Huenda huna ajira kabisa na unafikiria ukishapata ajira basi maisha ndiyo yataanza.
Inawezekana bado hujaingia kwenye biashara, na unachofikiria ni kwamba ukianza tu biashara, basi ndiyo maisha yako yanaanza.
Au pia bado hujaingia kwenye ndoa, na unachofikiria ukishaingia kwenye ndoa basi ndiyo maisha yameanza…
Chochote ambacho unafikiria kikishatokea au kukamilika ndiyo maisha yameanza, unajidanganya.
Maisha ndiyo hayo uliyonayo sasa, pale ulipo sasa ni kipindi cha maisha yako, kama ulivyo ukurasa wa kitabu. Unapaswa kuishi maisha yako kwa ukamilifu kwa kila kipindi.
Kwa sababu yapo mambo ya kufanyia kazi na kujifunza kwenye kila hatua ya maisha, ambayo yatakuandaa kwa hatua nyingine ya maisha inayofuata.
Lakini kama utaendelea kuangalia hapo ulipo kama unapita tu, kama utaendelea kuona bado unajiandaa kuishi, hakuna wakati ambao utajiona umeshakuwa tayari kuishi.
Kwa sababu hicho unachosubiri kwa hamu, kitakuja kweli, lakini kitakuwa na changamoto zake na utajiuliza, hivi ndiyo nilikuwa nasubiria hichi kweli? Hakuna zaidi? Na hapo unaanza kuhangaika tena, huku ukiahirisha maisha.
Maisha ni hapo ulipo sasa, hayo ndiyo maisha yako kamili, yaishi leo, ukijiandaa kuwa bora zaidi kesho. Lakini usiahirishe maisha ya leo kwa sababu unasubiria maisha ya kesho. Maisha ya leo hayatarudi tena, na maisha ya kesho huna uhakika nayo sana.
Ishi leo, ishi sasa, usiahirishe sehemu yoyote ya maisha yako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.