Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera sana kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu TUKIO MOJA….
Mambo mengi yanayodumu kwenye maisha, huwa hayasababishwi na tukio moja pekee.
Iwe ni mafanikio au matatizo, huwa yanatokea matukio mengi yanayojirudia rudia ndiyo yanazalisha matokeo husika.
Lakini watu wengi utawaona wakikaza a kutafuta tukio moja ambalo litabadili kabisa maisha yao.
Wengi wanafikiri kipo kitu kimoja pekee ambacho wakishakijua au wakishaifanya, basi watapata kila wanachotaka.
Ukiondoa ajali, mambo mengine yote kwenye maisha yanatokana na matukio madogo madogo yanayoirudia rudia kwenye maisha yetu.
Hivyo badala ya kukazana kutafuta tukio moja litakalokufikisha unakotaka, hebu angalia ni matukio gani madogo madogo unapaswa kuyafanya kwa kujirudia ili kufika unakotaka kufika.
Ukishayajua matukio hayo, anza mara moja na usipoteze muda kusema kwamba unajiandaa au kusubiri tukio kubwa.
Uhuru wa kifedha unatengenezwa kwa namna mtu anavyotumia kipato chake kila siku, kiasi anachoweka akiba na kuwekeza. Usisubiri ushinde bahati na sibu ili kupata uhuru wa kifedha, anza na fedha unayopata kila wakati.
Afya bora inatokana na vyakula tunavyokula, mazoezi tunayofanya na namna tunavyojikinga na magonjwa kila siku. Usitegemee tukio moja pekee likabadili kabisa afya yako, labda kwa ajali, lakini kwa hali ya kawaida, lazima uweke kazi kila siku.
Usikazane kutafuta tukio moja, bali weka juhudi kila siku kwenye matukio mengi madogo madogo.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.