Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu DUNIA HAITASIMAMA….
Yawezekana una hofu nyingi sana kuhusu maisha na mambo yanavyokwenda..
Yawezekana usiku hupati usingizi kila ukifikiri namna maisha yanavyokwenda.
Yawezekana una madeni ambayo unaona kama ni mzigo mkubwa kwako.
Yawezekana wapo watu ambao wanakusumbua na unaona kama maisha ni kisirani.
Pamoja na hayo yote, nataka nikuambie kitu kimoja, iwapo utakufa leo, dunia haitasimama. Dunia itaendelea kwenda kama inavyokwenda.
Hofu, shida, changamoto, na hata madeni yako yote, hayataifanya dunia isimame, kwa sababu wewe haupo na ulipaswa kuhangaika nayo.
Hivyo basi rafiki, pamoja na yote unayopitia, pata muda wa kuishi, pata muda wa kufurahia maisha.
Pata muda wa kushukuru kwa kuwa hai leo,
Pata muda wa kushukuru kwa kuwa na watu ambao wanakujali.
Na pata muda wa kuwa na njia ya kuendesha maisha , hata kama ni ngumu.
Pata muda wa kushukuru kwa pumzi unayovuta bila shida yoyote, kwa sababu wapo wengi hawawezi kuvuta pumzi hii bure kabisa kama ufanyavyo wewe.
Jipe dakika chache, za kukaa, kuisahau dunia na matatizo yake, na pumua.
Jikumbushe kwamba, lolote linalokusumbua na kukufanya uwe na hofu leo, mwisho wake ni wewe ukifa.
Dakika chache za kukaa kimya, kufuta mawazo yote na kuvuta pumzi kwa kina, zitakuwa za maana kwako kwa siku yako nzima.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.