Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, nafasi bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu THAMANI IPO KWENYE KUPOTEZA…
Kuna vitu kwenye maisha yetu, ambavyo tunavichukulia kawaida sana wakati tunavyo, lakini vikishapotea ndiyo tunagundua thamani yake halisi.
Labda ni kazi ambayo unaona haikupeleki kokote, ambayo unaiona ni kikwazo kwako, lakini siku inapopotea, ndiyo unagundua ilikuwa na thamani fulani kwako.
Yawezekana pia ni biashara ambayo umekuwa unaifanya, yenye changamoto na wewe kuona haikupeleki kokote. Lakini unapoachana na biashara hiyo, ndiyo unagundua ilikuwa na kitu kwako.
Wakati mwingine tunatumia tu muda wetu hovyo kwa sababu tunao, kwa sababu tunauona. Lakini tukishaupoteza ndiyo tunagundua kwamba ulikuwa muda muhimu ambao hatukupaswa kuupoteza.
Wapo watu kwenye maisha yetu ambao tunawachukulia kawaida sana, tunaona wapo tu na hatuoneshi juhudi zozote za kuwathamini kwa namna wanavyopaswa kuthaminiwa. Ni mpaka pale tunapowapoteza, ndipo tunagundua thamani yao halisi, pale pengo lao linapoonekana na haliwezi kuzibika.
Hivyo rafiki, chochote ambacho unacho hapo ulipo, kithamini wakati unacho. Usisubiri mpaka kipotee ndiyo uanze kusema ningejua. Umeshajua sasa, chukua hatua.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.