Biashara yenye mafanikio inaendeshwa kwa mfumo. Mfumo wa biashara unakuwa na vipengele mbalimbali kama mauzo, masoko, uzalishaji, usimamizi na kadhalika. Kwa njia hii ya mfumo, mmiliki wa biashara anaweza kuiendesha vizuri biashara yake na kwa mafanikio makubwa sana.

Lakini mifumo yote ina changamoto kubwa moja, eneo moja likiwa na changamoto, linaathiri maeneo mengine yote. Yaani katika vipengele vyote vya mfumo, iwapo kipengele kimoja kitakuwa hakifanyi kazi vizuri, kinapunguza ufanisi wa vipengele vingine.

Ushauri

Kwa mfano pale ambapo eneo la masoko halifanyi vizuri, mauzo yanakuwa machache, haya yanapelekea mzunguko wa fedha kuwa mdogo na biashara kushindwa kujiendesha.

Biashara zote zinazoingia kwenye changamoto kubwa na hata kufa, matatizo yote huwa yanaanzia kwenye kipengele kimoja cha mfumo. Hapo ndipo mfumo mzima unaanza kupata shida na hatimaye biashara inashindwa kujiendesha.

Changamoto kubwa ni kwamba siyo rahisi kuona kwa haraka pale kipengele kimoja cha mfumo kinapoanza kuwa na changamoto. Wengi huona ni hali ya kawaida au hali ya mpito hivyo kuendelea kuwa na matumaini kwamba mambo yatakwenda vizuri.

SOMA; BIASHARA LEO; Kuwa Makini Unapoingia Kwenye Biashara Mpya, Hata Kama Umeshazoea Biashara…

Ni muhimu sana wewe kama mfanyabiashara, kujua ufanisi wa kila eneo la biashara yako. Jua kila eneo linachangiaje maendeleo ya maeneo mengine ya biashara yako. Hii itakusaidia kuona kwa haraka pale ambapo mambo hayaendi vizuri.

Usikubali eneo moja la biashara yako kuwa sababu ya kifo cha biashara yako nzima. Elewa changamoto za kila eneo la biashara na zifanyie kazi kabla hazijaleta madhara kwa biashara nzima.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog