#KURASA_KUMI ZA KITABU LEO.
KITABU; Philosophy for life and other dangerous situations : ancient philosophy for modern problems.
Kurasa 45 – 55

Jinsi ya kujijengea udhibiti binafsi (self-control).

Tafiti nyingi zinaonesha kwamba, watu wenye udhibiti binafsi wanakuwa na maisha bora na yenye mafanikio kuliko wale wanaokosa udhibiti binafsi.
Wanafalsafa wa kale walilielewa hili, hasa wastoa ambapo wapiweka mkazo sana kwenye mtu kuweza kujijengea udhibiti binafsi.
Udhibiti binafsi ni kiwango cha juu kabisa cha nidhamu binafsi, ambapo mtu unaziendesha hisia zako na siyo hisia kukuendesha wewe.

Katika kujijengea udhibiti binafsi, wastoa walipenda kutumia maeneo mawili makuu, chakula na vinywaji.
Katika kujijengea udhibiti binafsi, wastoa waliweza kukaa na njaa wakati wana chakula, au kukaa na kiu wakati maji wanayo.
Kwenda mbali zaidi kwenye kujijengea udhibiti, wastoa walipokuwa na kiu, walikunywa maji na kisha kuyatema.
Wastoa walisisitiza kula chakula cha kawaida kabisa hata kama wana uwezo wa kula chakula cha hadhi ya juu.
Waliaminu kwamba chakula ni kwa ajili ya kuupa mwili nguvu, na siyo kuridhisha ladha ya mdomo.

Mazoezi mengine ya udhibiti binafsi ambayo wastoa waliyafanya ni kama;
Kuvaa nguo za kawaida hata kama wana nguo nzuri.
Kulala chini hata kama wana vitanda vizuri.
Yote haya ni katika kuhakikisha wao ndiyo wanafanya maamuzi na siyo kuendeshwa na hisia zao.

Tunaweza kutumia mazoezi haya kujijengea udhibiti binafsi, ili tuache kufanya mambo kwa mazoea na kwa kuendeshwa na hisia na badala yake kufanya mambo kwa sababu ni muhimu na tumechagua kufanya.
Tukiweza kifikia ngazi hii ya udhibiti binafsi, hakuna kinachoweza kutuzuia kuishi yale maisha tunayotaka.

Kocha Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa