Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa na kuweza kupata makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu SULUHISHO LA MUDA MFUPI…
Kwenye kila jambo ambalo unapitia kwenye maisha yako, iwe ni changamoto, matatizo au uhitaji, kuna suluhisho la muda mfupi na suluhisho la muda mrefu.
Suluhisho la muda mfupi ni rahisi kufanyia kazi, matokeo yake siyo mazuri na yanadumu kwa muda mfupi mno.
Suluhisho la muda mfupi mara nyingi huwa ni kitu cha kufanya mara moja, ambacho hakiondoi tatizo bali kulihamisha kwa
Suluhisho la muda mfupi mara nyingi huwa ni kitu cha kufanya mara moja, ambacho hakiondoi tatizo bali kulihamisha tatizo hilo kwa muda tu.
Kwa upande wa pili lipo suluhisho la muda mrefu. Hili ni suluhisho ambalo linatoa majibu ya uhakika ya kutatua chochote. Suluhisho hili linahitaji muda, lina ugumu kufanya na ni kitu ambacho utahitaji kufanya kila siku.
Kwa mfano, changamoto ni kipato hakitoshi;
Suluhisho la muda mfupi ni kukopa, lakini tatizo lipo pale pale na mbaya zaidi unapokopa unaliongeza.
Suluhisho la muda mrefu ni kudhibiti matumizi na kuongeza kipato. Kila siku utahitaji kuweka juhudi mpaka kweli uongoke kwenye changamoto hiyo.
Wakati wowote, chagua suluhisho la muda mrefu, hili ndiyo linakufikisha kwenye mafanikio ya kweli.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.