Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunaweza kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NIFANYE AU NISIFANYE…

Watu wengi hushindwa kufanya maamuzi wanayoweza kuyafuata ya labda kufanya au kutokufanya kitu fulani.

Na wengi wanapofika kwenye maamuzi, wanakuwa tayari wamechoka na hawana tena nguvu za kuweza kufanya.

Wengi wamekuwa wakikwama njia panda ya KUFANYA au KUTOKUFANYA.

Wengi wamekuwa wanajiuliza swali hilo na kuanza kupitia kila upande, je iwapo akifanya faida ni zipi na hasara ni zipi. Na asipofanya faida ni zipi na hasara ni zipi.

Ingekuwa vyema kama mtu angejumlisha hizo faida na hasara na kisha kufanya maamuzi. Lakini mjadala huendelea zaidi. Kwenye kila faida na kila hasara inahojiwa tena na tena.

Kwa kifupi mtu anakuwa anatumia muda na nguvu nyingi kushindana na yeye mwenyewe iwapo afanya au asifanye. Zoezi hilo linamchosha sana kiasi kwamba baada ya muda anashindwa kujua hata maamuzi mazuri kwake ni yapi.

Wengine hufanya maamuzi labda ya kufanya, lakini wanapoanza kufanya, wanaanza kujikumbusha tena sababu za kwa nini wasifanye. Hapo wanaacha kufanya na kurudi tena kwenye mjadala iwapo wafanye au wasifanye.

Sasa rafiki yangu, okoa muda na nguvu zako kwa kufanya maamuzi mara moja kulingana na faida na hasara unazoweza kufikiria. Ukishafikia maamuzi unafanya, basi futa kabisa mjadala huo na anza kufanya. Na fanya mpaka utakapopata matokeo unayotaka.

Kadhalika kama umeamua usifanye, hamishia mawazo yako na nguvu zako kwenye vitu vingine. Usianze kurudi tena na kujiuliza au labda ningefanya.

Mara nyingi maamuzi tunayofanya mara ya kwanza, hata kama baadaye tunakuwa na wasiwasi nayo, huwa ndiyo maamuzi sahihi. Hivyo fanya maamuzi na chukua hatua.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz