Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi kubwa na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunaweza kwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUPENDA UHAKIKA…
Kuna watu ambao wamekaa mahali ambapo hawanufaiki kabisa, lakini hawaondoki kwa sababu ya uhakika ambao wameshajitengenezea.
Kwa mfano inaweza kuwa kazi ambayo haimridhishi mtu, kipato ni kidogo na hakitoshelezi, lakini ule uhakika ambao mtu ameshauzoea, wa kila mwisho wa mwezi kupata mshahara, unamfanya asifikirie kitu kingine.
Au inaweza kuwa biashara ambayo ni ndogo, haikui na kipato chake siyo kikubwa. Lakini unakuta mtu anaifanya vile vile kwa kiwango kile kile. Hajaribu mambo mapya na makubwa kwa sababu ameshazoea ule uhakika ambao anapata sasa.
Kupenda uhakika ni adui mkubwa wa mafanikio makubwa.
Unapofanya kile tu ambacho umezoea kufanya, unapata matokeo yale ambayo umekuwa unapata mara zote.
Mafanikio yetu, yapo nje ya uhakika, yapo kwenye kufanya mambo ambayo hatujazoea kufanya, mambo ambayo ni makubwa na yenye uwezekano wa kushindwa.
Ni huo uwezekano wa kushindwa ambao unawafanya watu kupenda kile ambacho wana uhakika nao.
Na hapo ndipo wewe unapaswa kujitofautisha nao. Kwa kuwa tayari kujaribu vitu vipya, kufanya vitu ambavyo hujazoea kufanya, ili kuweza kupata matokeo makubwa.
Nenda kabadili kitu leo rafiki yangu.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.