Mapinduzi makubwa sana yameshafanyika kwenye biashara kwa ujio wa mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii. Sasa hivi nguvu kubwa ipo kwa wateja na siyo wafanyabiashara.
Siku za nyuma ilikuwa kampuni inaamua izalishe nini, kisha inatengeneza matangazo yenye kuvutia sana na kuwashawishi watu mpaka wapokee ile bidhaa inayotolewa.
Lakini sasa hivi mambo yamebadilika. Sasa hivi mawasiliano baina ya watu wa sehemu mbalimbali yamerahisishwa sana na mitandao ya kijamii. Kama watu hawaridhishwi na jambo lolote, wana nafasi ya kulisema haraka na kupata suluhisho au mbadala kutoka kwa wengine.

Ulimwengu wa sasa wa mitandao ya kijamii, watu wanashirikishana maoni yao na kila mtu ana maoni yake kwenye kila jambo. Uhuru wa maoni na kujieleza umekuwa dhahiri kipindi hichi.
Hivyo badala ya kupambana kutaka kuwapa kitu unachotaka wewe, ni vyema kusikiliza. Ni vyema kuangalia maoni ya watu kuhusiana na bidhaa au huduma fulani yapoje. Kisha wewe ukaangalia hatua zipi unaweza kuchukua za kuboresha zaidi.
Sikiliza watu wanasemaje kuhusiana na biashara yako, wasikilize wanasemaje kuhusiana na washindani wako wa kibiashara. Pia sikiliza wanasema kuhusu biashara kwa ujumla.
Wanaweza wasiwe sahihi kwa maoni yao, ila kutokuwasikiliza utakuwa umejinyima fursa nzuri na ya kipekee kwako.
Tupo kwenye zama za wateja kuwa na nguvu kubwa juu ya mahitaji yao na huduma wanazotaka. Kusikiliza kutakuwezesha kuwasaidia na kuwafikia wateja wengi zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog