KITABU; Philosophy for life and other dangerous situations : ancient philosophy for modern problems / Jules Evans
UKurasa 123 – 132.

Sehemu kubwa ya yale ambayo tunayafanya kwenye maisha yetu, yanatokana na tabia na mazoea ambayo tumwjijengea.
Vitu vingi unafanya bila hata ya kufikiri.
Na hata namna tunavyofikiri ni kwa mazoea.
Tunapokutana na jambo lolote, akili zetu zinafikiri kwa haraka kwa namna tulivyozoea.
Ili kuweza kufikiri kwa kina na siyo kwa mazoea, tunahitaji kutengeneza mazoea mapya kwenye akili zetu.
Njia ya kufanya hivyo ni kuwa na kauli au maelezo chanya ambayo mtu unayarudia kila mara mpaka uyakariri kabisa.
Ukishayakariri, unaanza kufanya kwa mazoea, lakini sasa ni mazoea mazuri na yenye manufaa.

Mwanafalsafa Pythagoras alikuwa mmoja wa watu waliotumia njia hii kuwajengea watu falsafa yake.
Watu walipewa maneno ya kurudia rudia na kukariri mpaka hata kwa kuimba.

Njia hii imeendelea kutumia na falsafa nyingine na hata dini pia.
Mbinu hii inafanya kazi kwa nguvu kubwa, lakini pia ni hatari kwa sababu ikifanywa bila ya kuzingatia umakini, inaweza kuwafanya watu kuwa wategemezi kwa wengine, kwa kushindwa kufanya maamuzi yao wenyewe.
Wapo watu wamekuwa wakitumia nguvu hii hasa kwenye dini na kuzalisha watu hatari sana.
Unaposikia mtu anaenda kujitoa mhanga, kujiua pamoja na watu, jua kabisa mtu huyo akili yake imeshaharibiwa kwa kujazwa vitu ambavyo vinamzuia yeye kufikiri kwa kina.

Tutumie nguvu hii kujitengenezea tabia mpya na nzuri. Lakini pia tuwe macho ili wengine wasiitumie kutulaghai na kukutapeli.

Kocha Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa