Katika kununua, watu wanaendeshwa na hisia zaidi ya fikra. Huwa tunafikiri kwamba watu watakuwa ‘logical’ katika kufanya maamuzi ya kununua, lakini huo siyo ukweli. Watu huwa wanaendeshwa na hisia zaidi katika kufanya maamuzi kuliko kufikiri kwa kina.

Na hapo ndipo wengi wanapokosea, kwa kuamini watu watanunua kile wanachouza, kwa sababu labda ni kizuri au wanakihitaji.

Lakini watu kabla hawajanunua kile unachouza, wanakununua wewe kwanza. Na siyo kukununua kwa kukulipia fedha, bali kukununua kwa kukubali wewe. Watu wanapenda kufanya biashara na watu ambao wanawaamini, watu ambao wanawavutia na hapo ndipo wanakuwa na amani na utayari wa kununua.

jiuze wewe

Hivyo kwa biashara yoyote unayofanya, hakikisha unajiweka kwa njia ambayo unawavutia na kukubalika na ile aina ya wateja unaowalenga. Hakikisha unaaminika na unajenga mazingira ya urafiki na wateja wako.

Wateja wanajiona salama zaidi wanapoona wananunua kwa watu wanaowajali, kuliko wanapoona wananunua kwa mtu anayeangalia fedha pekee.

SOMA; BIASHARA LEO; Kabla Watu Hawajanunua Wanataka Hichi, Na Baada Ya Kununua Wanataka Hichi.

Jenga mazingira ya uaminifu kwenye biashara yako, mazingira rafiki. Wewe pamoja na wasaidizi wako kwenye biashara, tengenezeni mahusiano mazuri na wateja wa biashara yenu.

Wateja wanapowakubali, ninyi, inakuwa rahisi kwao kununua kwako kuliko wanapokuona uko pale kuuza pekee.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog