Soko la hisa limegawanyika kwenye aina kuu mbili, kulingana na hisa zinazouzwa sokoni.
Aina ya kwanza ni soko la awali (primary market). Hili ni soko la hisa ambapo hisa ndiyo zinaingia sokoni kwa mara ya kwanza. Hapa kampuni au taasisi inakuwa ndiyo inaandikisha hisa zake kwenye soko la hisa. Katika kipindi hichi, bei ya hisa inapangwa na kampuni yenyewe, kulingana na thamani waliyoipiga wao kwa kampuni yao. Fedha zote ambazo zinapatikana katika kipindi hichi, zinatumiwa na kampuni katika shughuli zake.
Zoezi la kuuza hisa kwa mara ya kwanza huitwa Initial Public Offering (IPO) na hapa kampuni inakuwa inauza hisa zake kwa wawekezaji.
Kununua hisa wakati huu kuna faida na hatari zake. Faida ni kwamba hisa zinaweza kuwa bei chini wakati wa soko la awali, na zinapoingia sokoni bei yake ikapanda. Hivyo mtu anayenunua kwenye soko la awali anaweza kunufaika hisa zinapoingia sokoni rasmi.
Hasara ni kwamba hisa zinaweza kushuka bei zikishaingia sokoni, na hapo mtu anaweza kupata hasara kama alikuwa anategemea anunue na kuuza haraka. Lakini kama mtu akiwa na subira, hisa huja kupanda bei baadaye.

Aina ya pili ya soko la hisa ni soko la upili (Secondary Market). Hapa hisa zinakuwa zimeandikishwa kwenye soko la hisa na watu wananunua na kuuza kutoka kwa wawekezaji wengine. Katika soko hili la upili, bei ya hisa inategemeana na mwenendo wa uchumi na hata ufanisi wa kampuni husika. Katika soko la upili, hisa hupanda na kushuka bei kulingana na mabadiliko yanayotokea.
Fedha za mauzo na manunuzi ya hisa kwenye soko la upili haziendi moja kwa moja kwenye kampuni husika kama ilivyokuwa kwenye soko la awali. Badala yake hisa zinabadilishwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Katika soko la upili, wawekezaji wanauza hisa kwa wawekezaji wengine.
SOMA; UWEKEZAJI LEO; Faida Tano Za Kununua Na Kuwekeza Kwenye Hisa.
Faida ya soko la upili ni kuweza kupata hisa kwa bei rahisi, hasa pale kunapokuwa na changamoto za kiuchumi. Kama ni mfuatiliaji mzuri wa soko la hisa, unaweza kuona hisa ambazo zina bei ndogo lakini thamani ya kampuni husika ni kubwa. Ukinunua hizo unanufaika sana baadaye.
Hasara ya soko la upili ni kuchelewa pale hisa zinapokuwa na bei ndogo kwenye soko la awali, na bei kupanda zinapoingia sokoni.
Kuelewa aina hizi mbili za soko la hisa kunakuwezesha kuchukua hatua, hasa pale unaposikia hisa fulani zinaingia sokoni kwenye soko la awali. Hapo unaweza kufanya maamuzi sahihi ya kununua au kusubiri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog