Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo TUTAFAKARI na KUTAHAJUDI kuhusu KINACHOTOKEA SASA…
Kila mmoja wetu ana wakati uliopo, wakati ambao tunao sasa. Sasa hivi wakati unasoma hapa, au unafanya chochote unachofanya sasa.
Wakati ulionao sasa, ni wakati wa thamani sana kwako. Ni wakati pekee ambao unauishi, na ni wakati unaoweza kuchukua hatua ili kubadili na kuboresha maisha yako kwa wakati ujao.
Kitu ambacho wengi hatuelewi ni kwamba, chochote kinachotokea sasa, hatuwezi kukibadili sasa. Hakuna namna tunaweza kuzuia kile ambacho tayari kinatokea. Badala yake tunaweza kuchukua hatua leo na kubadili kile kinachokuja kutokea.
Sasa watu wengi wanateseka na maisha, kupata msongo wa mawazo na hata sonona kwa sababu wanakazana kubadili kile ambacho kinatokea sasa. Hii ni swala na nyumba inayowaka moto, halafu mtu anataka azime moto huo na kusiwe na uharibifu wa aina yoyote. Haiwezekani.
Kinachotokea sasa, ndiyo kimeshapangwa kutokea, huenda wewe mwenyewe umeshiriki kutengeneza kinachotokea sasa, au umeruhusu kitokee kwa sababu hukushiriki kuzuia kisitokee.
Kushindana na kinachotokea sasa hakuwezi kukusaidia kwa lolote, kwa sababu hakutazuia kinachotokea. Njia bora ni kukubali kinachotokea na kuchukua hatua kubadili kinachokuja kutokea, wakati ujao. Lakini kumbuka, kubadili kinachokuja, hatua unachukua sasa.
Ishi sasa, kubali kinachotokea na tumia muda huu kuchukua hatua kubadili kinachokuja.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.