Wengi wetu tunaposikia neno dalali tunajua ni mtu ambaye anafanya biashara ya kuuza vitu vya wengine, kwa kuongeza bei ili apate fedha. Kwa fikra hizi tuna mtazamo mbaya kuhusu madalali na kuona ni watu wanaolangua wengine.

Hivyo tunaposikia tena kwenye soko la hisa kuna madalali, tunastuka na kukosa amani. Tunajiuliza tutakuwaje na uhakika na hawa madalali? Je hatuwezi kutapeliwa? Na je unachaguaje dalali mzuri na mwaminifu?

Stock

Haya yote tutakwenda kujifunza kwenye makala ya leo.

Dalali wa hisa ni mtu wa aina gani?

Dalali wa hisa, ni kampuni ambayo inajihusisha na kuwawezesha watu kuuza na kununua hisa. Kama tunavyojua, soko la hisa ni kubwa, na haiwezekani kila mtu akashiriki moja kwa moja kununu au akuuza hisa zake.

Hivyo unapotaka kununua au kuuza, unapitia kwa dalali, ambaye anachukua mahitaji yako na kushiriki sokoni kwa niaba yako.

Madalali hawa siyo kama wa mtaani, wale ambao wanaweza kuongeza bei jinsi wanavyojisikia wao wenyewe. Bali wanatabulika kisheria na wanasimamiwa na sheria.

Kampuni za udalali kwenye soko la hisa zinatambuliwa kisheria na zinafanya mengi zaidi tu ya kuuza na kununua hisa. Wanatoa elimu ya uwekezaji, wanatoa ushauri wa uwekezaji na pia wanayasaidia makampuni yanayohitaji kujiandikisha kwenye soko la hisa.

Hivyo hupaswi kuwa na wasiwasi unapojihusisha na madalali wa soko la hisa, muhimu tu iwe ni kampuni ambayo imeorodheshwa na soko la hisa kwamba ni madalali.

SOMA; Sheria Tano Muhimu Za Kufuata Wakati Wa Kuchagua Hisa Za Kununua.

Dalali wa soko la hisa analipwaje?

Kwa Tanzania, madalali wa soko la hisa wanalipwa kwa kamisheni kutokana na mauzo au manunuzi yako ya hisa. Kwenye ile fedha unayowekeza au unayopata baada ya kuuza hisa, dalali anakata asilimia yake. Mara nyingi ni asilimia chini ya mbili ya kiasi chote cha fedha.

Je unawezaje kuchagua dalali mzuri wa soko la hisa?

Hakuna tofauti kubwa baina ya madalali wa soko la hisa kwa upande wa gharama, yaani asilimia wanazotoza kwenye mauzo na manunuzi.

Bali tofauti zinaweza kuwepo kwenye urahisi wa kufanya kazi na dalali husika. Kwa mfano kuna madalali ambao wana mawakala maeneo mengi na ya mikoani.

Pia utoaji wa elimu na ushauri unaweza kutofautiana baina ya madalali, hivyo unaweza kuongea na baadhi yao na kuona wapi ambao wanakushauri vizuri kuhusu uwekezaji wako.

Mwisho kabisa ni huduma unazopata kutoka kwa dalali. Hizi pia zinatofautiana, wapo ambao wanakupa huduma nzuri, kukufuatilia vizuri mpaka unapokamilisha ununuzi au uuzaji wa hisa zako.

Je unaruhusiwa kutumia dalali zaidi ya mmoja?

Jibu ni ndiyo, unaweza kutumia dalali zaidi ya mmoja au hata kubadili dalali. Unapochagua kufanya kazi na dalali mwingine, ipo fomu ambayo unajaza na unaweza kununua au kuuza kupitia yeye.

Kujua orodha ya madalali wa soko la hisa la Dar, bonyeza maandishi haya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog