Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?

Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo ambapo tumepata nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MATARAJIO NA UHALISIA…

Kwenye kila jambo ambalo tunafanya kwenye maisha yetu, huwa tuna matarajio fulani.

Huwa tunatarajia kupata matokeo mazuri na makubwa ambayo yatatuwezesha kupiga hatua zaidi.

Lakini sasa unakuja uhalisia, ambao mara nyingi ni tofauti kabisa na matarajio.

Kile hasa tunachopata, huwa tofauti na kile ambacho tulitarajia kupata.

Na hii hupelekea wengi kuumia na hata kukata tamaa kwa kukosa kile ambacho walikuwa wanataka.

Ninachotaka uelewe rafiki ni kwamba, matarajio yoyote uliyonayo, jua uhalisia unaweza kuwa tofauti, na mara nyingi unakuwa tofauti.

Hivyo badala ya kuumia na uhalisia unaokutana nao, badala ya kuumia na matokeo unayopata, kazana kuweka juhudi kadiri ya uwezo wako.

Fanya kila unachoweza kufanya, nenda hatua ya ziada, kazana kuweka juhudi kubwa, halafu pokea matokeo unayopata. Ukishapata matokeo hayo, kazana kuyaboresha zaidi.

Hivyo ndivyo maisha yanavyokwenda, ukibaki unalalamika na matokeo au uhalisia uliokutana nao, hutaweza kupiga hatua kwenye maisha yako.

Pambana na kile unachoweza kudhibiti, kile ambacho kipo ndani ya uwezo wako, ambacho ni juhudi unazoweka. Matokeo hayapo ndani ya uwezo wako, pokea kadiri unavyopata na endelea kuweka juhudi.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz