KITABU; Philosophy for life and other dangerous situations : ancient philosophy for modern problems / Jules Evans
UKurasa 227 – 236.

Falsafa zote na hata imani za kidini, zinaweka mkazo kwenye kitu kimoja, kwamba sisi ni zaidi ya hii miili tunayoiona.
Ndani yetu kuna kitu kikubwa sana, ambacho ndiyo kinabeba maana ya maisha yetu.
Ndani yetu tuna roho, ambayo hii inatuunganisha na dunia nzima, na kwa kila aina ya falsafa, inaeleza roho hii huwa haifi, bali inaendelea kuishi.

Kitu kikubwa ambacho wanafalsafa wanatukumbusha ni kwamba, majawabu ya matatizo na changamoto zote tunazopitia yapo ndani ya roho zetu.
Pia wanatuambia kwamba zoho hizi zimekamilika, zina kila tunachohitaji, ni swala la sisi kuuliza na kupata majibu.

Mwanafalsafa Montaigne anasema kwamba sisi wote ni matajiri kuliko tunavyofikiri, lakini tumefundishwa kukopa na kuwa ombaomba kwa wengine, lakini pia tunahitaji mambo madogo sana ili kuwa na maisba mazuri.

Wastoa wanatuambia, mahitaji yetu ya msingi kabisa ni machache sana, lakini sisi tunayakuza mpaka yanakuwa nje ya uwezo wetu na tunateseka nayo.

Tunapokutana na changamoto na matatizo kwenye maisha yetu, tukumbuke kurudi ndani yetu, kupata muda tulivu, wa kukaa na kutafakari, kuuliza nafsi zetu na kupata majibu ya uhakika.
Pia tuishi yale maisha ambayo tunapata kila ambacho ni muhimu kwetu, kabla hatujakimbikia yale yaliyopo nje ya uwezo wetu.

Na huu ndiyo mwisho wa KITABU; Philosophy for life and other dangerous situations : ancient philosophy for modern problems ambacho kimetufundisha falsafa mbalimbali za kale ambazo tunaweza kuzitumia kwenye nyakati ngumu za maisha yetu.
Falsafa hizi ni za miaka mingi, lakini misingi yake ipo sahihi mpaka sasa. Na hii ni sababu kubwa kwetu kuzitumia katika kutatua changamoto za maisha yetu ya kila siku.
Tumejifunza kutoka kwa Socrates, Plato, Aristotle, Seneca, Marcus Aurelius, Epicurus, Epictetus na wanafalsafa wengine wengi.
Kuchagua kuishi maisha ya falsafa na misingi yake, ni kuchagua kuishi maisha mazuri na yenye maana kwako na wale wanaokuzunguka.

Kocha Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa