Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HATA KAMA HAKUNA ANAYEKUONA…
Watu wengi huwa makini sana na mambo wanayofanya pale ambapo wanaonekana na wengine.
Lakini wanapokuwa wenyewe, wanapokuwa faragha hufanya mambo ya tofauti kabisa, mambo ambayo wasingependa wengine wayaone.
Sasa hali hii imekuwa inawajengea watu hofu kwenye kila wanachofanya, hasa faraghani, wakijiuliza huenda wanaonekana na kila kitu kuwa wazi.
Kuondokana na hali hii na kuwa huru na maisha yako, ni vyema ukawa na maisha ya aina moja, kufanya jambo sahihi wakati wote, HATA KAMA HAKUNA ANAYEKUONA.
Na kwa dunia ya sasa, ni vyema ukafikiri kwamba kila unachofanya basi kila mtu anakiona, kwa sababu kwa namna yoyote ile, yupo mtu anayekuona. Na akikuona mmoja, anakurekodi kabisa, hivyo dunia nzima ina uwezo wa kukuona.
UADILIFU ni kufanya jambo sahihi hata kama hakuna anayekuona. Ndiyo maana uadilifu utakusaidia sana kuwa na maisha bora, kwa sababu hutakuwa ukijidanganya na kujaribu kuwadanganya wengine.
Fanya jambo sahihi mara zote, HATA KAMA HAKUNA ANAYEKUONA, kwa sababu ukweli ni kwamba, kila mtu anakuona, ni wewe tu hujajua.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.