KITABU; Socrates’ way : seven master keys to using your mind to the utmost / Ronald Gross.
UKURASA; 91 – 100
Socrates alijenga sifa yake kupitia kufikiri kwa kina na kuuliza maswali mazuri.
Hivi ni vitu viwili vinavyokosekana kwenye zama tunazoishi sasa, watu hawafikiri, wanapokea kila wanachoambiwa, kama kilivyo.
Watu pia hawahoji wala kuuliza maswali.
Wanafalsafa walioshika misingi ya Socrates kama Dr Edward Bono wametushirikisha mbinu saba za kufikiri vizuri.
Mbinu hizo ni kama ifuatavyo;
- Faida, Hasara na cha kupendeza.
Kila jambo lina faida na hasara zake, lakini pia kuna kitu cha kupendeza au la kuvutia kwenye kila jambo. Badala ya kuangalia faida na hasara pekee, angalia pia kipi cha kupendeza au kuvutia kwenye jambo husika. -
Zingatia mambo yote yanayohusika.
Kwenye kila jambo unalofikiria, mambo mengi huwa yanahusika. Wengi hawapendi kujisumbua hivyo hufikiri yale machache pekee. Wewe usiwe na haraka, zingatia kila jambo linalohusika, utapata picha kamili. -
Matokeo na mwendelezo.
Kwa maamuzi yoyote utakayochukua, kuna matokeo ya haraka na matokeo ya muda mrefu. Zingatia yote hayo kwa kufikiria miaka mingi inayokuja kwa maamuzi unayotaka kufanya. -
Makusudi, malengo na matokeo.
Mara nyingi watu huangalia eneo moja pekee, kutimiza lengo fulani wanalotaka kutimiza. Hii hupelekea wao kutokuona kusudi kubwa la kufanya kile wanachofanya, au kufikiria matokeo wanayozalisha.
Usiangalie malengo yako pekee. -
Vipaumbele muhimu vya kwanza.
Kwa kuwa kutakuwa na mambo mengi ya kufanya, lazima uwe na vipaumbele, ujue yapi muhimu kuanza kabla ya mengine. -
Machaguo mbadala.
Hata baada ya kufikia maamuzi ya kipi unakwenda kufanya, angalia pia machaguo mbadala. Kipi tofauti ungeweza kufanya, hapo utaweza kupata uelewa mkubwa zaidi. -
Mtazamo wa tofauti.
Hatua zote hizo zinakupelekea wewe kuona kitu kwa mtazamo wa tofauti. Tofauti na vile ambavyo wengi wanapenda kufikiri kwa mazoea.
Kila unachofikiri, angalia na mtazamo wa tofauti, tofauti na kile unachofikiri wewe.
Tutumie mbinu hizi saba kufikiri vizuri.
Kocha Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa